Baba mzazi wa Samatta afariki Dunia

Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa familia, Mzee Samatta alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya kwa hivi karibuni.
NI huzuni kubwa katika familia ya mshambuliaji wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta 'Samagol' kufuatia taarifa za kifo cha baba mzazi, Ally Pazi Samatta.
Mzee Samatta amefariki dunia asubuhi hii ya Jumapili akiwa nyumbani kwake Mbagala Dar es Salaam na taarifa za kifo chake zimethibitishwa na mwanae, Mohamed Samatta.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa familia, Mzee Samatta alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya kwa hivi karibuni.
"Mzee amefariki leo nyumbani hakuwa ameugua kwa muda mrefu na juzi aliniambia njoo mwanangu unione daah! Ndio hivyo tena," amesema mmoja wa ndugu wa karibu wa familia hiyo.
Mzee Samatta enzi za uhai wake alikuwa ni mshambuliaji nyota aliyewahi kutamba na klabu kadhaa na kuichezea timu ya taifa, akivaa jezi namba 10 na alikuwa mtu mashuhuri katika jamii yake, akiheshimika kwa malezi bora aliyowapatia watoto wake, hasa Mbwana ambaye amekuwa nembo ya soka la Tanzania kimataifa.
Marehemu aliwahi kuelezea namna alivyomlea mwanawe katika maadili, nidhamu na upendo na kulitumikia taifa lake, mambo ambayo bado yanaonekana katika mwenendo wa nyota huyo wa soka.
Ni pengo kubwa kwa familia, lakini pia kwa taifa ambalo limemshuhudia baba huyo akiwa bega kwa bega katika mafanikio ya mwanaye uwanjani. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.