Barcelona yaendelea kugawa dozi Hispania

Muktasari:
- Barcelona imeendelea kupata matokeo mazuri baada ya kutoka kuifunga Real Madrid mabao 5-2 kwenye mchezo wa fainali ya Super Cup uliopigwa Januari 12, 2025, nchini Saudi Arabia.
Barcelona imeendelea kuonyesha makali yake baada ya kupata ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Real Betis katika mchezo wa Kombe la Mfalme (Copa del Rey), uliopigwa kwenye Uwanja wa Lluís Companys Olympic ambao Barca inautumia kama uwanja wa nyumbani.
Barcelona ilianza kupata bao dakika ya tatu likifungwa na Gavi ambaye alipewa pasi ya mwisho na Dan Olmo. Bao la pili lilifungwa na Jules Counde dakika ya 27 akiunganisha pasi aliyopewa na Lamine Yamal.
Dakika ya 58, Raphinha alifunga bao la tatu kabla ya Ferran Torres kuandika la nne dakika ya 67 akiunganisha pasi ya Dan Olmo kwa kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Betis, Fran Vieites.
Barcelona ilipata bao la tano dakika ya 75 likifungwa na Yamal ambaye amezidi kuonyesha kiwango bora kila kukicha baada ya kutoka kufunga bao siku chache zilizopita dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
Real Betis ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Vitor Roque dakika ya 84 ambaye alipiga mkwaju wa penalti baada ya Jules Counde kumchezea vibaya mshambuliaji wa Betis Jesus Rodriguez ndani ya eneo la hatari.
Barcelona imeendelea kupata matokeo mazuri baada ya kutoka kuifunga Real Madrid mabao 5-2 kwenye mchezo wa fainali ya Super Cup uliopigwa Januari 12, 2025, nchini Saudi Arabia.
Baada ya mchezo wa jana kumalizika Barcelona itasafiri kwenda ugenini kuikabili Getafe katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) wakati Real Betis itakuwa nyumbani ikiikaribisha Alaves.