Bayern Munich yafanya mauaji, yaitandika Bremer mabao 12-0

Muktasari:
- Eric Maxim Choupo-Moting jana amefunga mabao manne wakati vigogo wa ligi ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich walipotoa kipigo cha mabao 12-0 dhidi ya timu ndogo ya Bremer 12-0 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Ujerumani.
Berlin, Ujerumani (AFP). Eric Maxim Choupo-Moting jana amefunga mabao manne wakati vigogo wa ligi ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich walipotoa kipigo cha mabao 12-0 dhidi ya timu ndogo ya Bremer 12-0 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Ujerumani.
Awali mechi hiyo iliahirishwa mwanzoni mwa Agosti baada ya wachezaji wa Bremer kupata maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona, Uviko-19.
Bremer inacheza ligi ya mkoa, lakini Bayern haikuonyesha huruma kubwa.
Ilikuw ainaongoza kwa mabao 8-0 wakati Bremer ilipompoteza beki Ugo Nobile, aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwa kumuangusha chini kiungo Michael Cuisance aliyekuwa akielekea kufunga zikiwa zimesalia dakika 13.
Licha ya mshambuliaji wao nyota, Robert Lewandowski na kipa wa Ujerumani, Manuel Neuer kupumzishwa, Bayern ilifanya mauaji yaliyoipeleka katika raundi inayofuata ambayo ratiba yake itapangwa Jumapili.
Choupo-Moting alifunga mabao yake matatu ndani ya dakika 35 za kwanza, na akiwa amepewa kitambaa cha nahodha katika kipindi cha pili, alifunga bao lake la nne na la kumi kwa Bayern katika dakika za mwisho.
"Tulipambana kuanzia mwanzo hadi dakika ya mwisho, ndio maana mechi ilikuwa namna hiyo," alisema.
Winga wa Ujerumani, Leroy Sane alimrahisishia kazi Choupo-Moting kufunga mabao yake mawili ya kwanza alipompa pasi zilizomfanya abakie na jukumu la kugongea mpira wavuni, kabla ya nyota huyo wa Cameroon kufunga kwa kichwa bao la tatu baada ya ngome ya wapinzani kushindwa kuokoa mpira.
Nyota wa zamani wa timu ya vijana ya England na sasa kiungo wa timu ya taifa ya Ujerumani, Jamala Musiala, 18, alihusika katika mabao mawili ya kipindi cha kwanza, na baadaye akafunga katika kipindi cha pili.
Alipiga kiki akiwa pembeni ya lango na baadaye kuubetua mpira kumpita kipa wa Bremer huku juhudi za kuokoa za beki Jan-Luca zikisaidia kuuingiza wavuni.
"Ilikuwa raha kufunga mabao na kucheza kwa mtiririko," alisema Musiala.
Hadi mapumziko Bayern ilikuwa inaongoza kwa mabao 5-0, lakini ikaongeza mengine mawili kwa haraka wakati mchezaji mwenye umri wa miaka 19, Malik Tillman alipotumia makosa ya mabeki kabla ya Musiala kufunga bao lake la pili.
Kocha wa Bayern, Julian Nagelsmann alifanya majaribio kwa kumpa nafasi beki wa kushoto, Omar Richards kucheza mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe kutoka Reading mwezi uliopita.
Beki wa Marekani, Chris Richards, 21, pia alichezeshwa baada ya kuingia kipindi cha pili.