Bodi inavyochuma mamilioni ya klabu
Dar es Salaam. Kwa kipindi cha miezi sita tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara Septemba 17, 2025, taswira ya ushindani imeambatana sambamba na wimbi kubwa la faini kutoka Kamati ya Nidhamu ya Bodi ya Ligi (TPLB).
Wakati mashabiki wakifurahia burudani ya soka kila wiki, nyuma ya pazia kumekuwa na rungu la adhabu kwa klabu zinazokiuka kanuni baada ya michezo 15 tu kuchezwa.
Kwa jumla, klabu 13 kati ya 16 za ligi ambayo inaongozwa na Yanga yenye pointi 38 kileleni zimejikuta zikilipa kiasi cha Sh202 milioni, huku wachezaji wakilipa Sh17.2 milioni, hali inayodhihirisha wazi kuwa changamoto za kidhamu ni kubwa kwenye soka letu kwa sasa.
Kiasi hiki sio kidogo, hasa ukizingatia kuwa ni fedha ambazo zingeweza kuelekezwa katika maendeleo ya timu lakini badala yake zimeishia kulipia makosa yanayoweza kuzuilika.
Kinara wa orodha ya faini ni Simba pamoja na Dodoma Jiji FC, kila mmoja akifikisha Sh30 milioni, jambo linaloonyesha kuwa hata klabu kubwa au zenye uzoefu haziko salama dhidi ya makosa ya kinidhamu.
Zinafuatiwa na TRA United Sh25 milioni na Mtibwa Sugar Sh25 milioni, ambazo pia zimeathirika kwa kiasi kikubwa rungu hilo la kamati ya bodi ya Ligi huku mabingwa watetezi, Yanga nao wakilipa Sh20 milioni.
Kwa upande mwingine, kuna klabu ambazo hazijaguswa kabisa na kamati hiyo ambazo ni JKT Tanzania FC, Singida Black Stars na Mbeya City FC, zikionesha mfano kwamba nidhamu inawezekana.
Chanzo kikubwa cha faini hizi kimekuwa ni kushindwa kufuata kanuni za msingi za uendeshaji wa timu, ambapo suala la makocha wasio na vigezo limeonekana kuzigharimu Mtibwa Sugar FC, TRA United SC na Dodoma Jiji FC.
Katika hilo, Mtibwa Sugar ililimwa Sh20 milioni kwa kufanya hivyo katika mechi nne tofauti za Ligi Kuu Bara huku TRA United na Dodoma Jiji kila mmoja akitozwa Sh15 milioni kwa kosa hilo katika mechi tatu.
Hii inaashiria tatizo la msingi katika uwekezaji wa kiufundi ndani ya klabu, kwani katika soka la kisasa, kocha ni nguzo muhimu ya mafanikio na sio suala la kuchukulia poa.
Mbali na hilo, utovu wa nidhamu wa mashabiki nao umeendelea kuwa chanzo kikubwa cha adhabu, hasa kwa klabu kubwa kama Simba na Yanga.
Matukio ya kurusha chupa uwanjani, kuvamia uzio, pamoja na vitendo vinavyohusishwa na imani za kishirikina kama kutumia milango isiyo rasmi na kumwaga vimiminika, yamezigharimu klabu hizi fedha nyingi.
Kwa upande wa Simba matukio ya mashabiki yamewagharimu kiasi cha Sh 10 milioni, jambo ambalo linaonekana kuwa hatari zaidi kwao.
Hali hii inaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuwaelimisha mashabiki kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kulinda taswira ya ligi, hasa katika zama hizi ambazo soka linatazamwa kimataifa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Pia, makosa yanayoonekana kuwa madogo kama kuchelewa kwa mechi au kutofuata taratibu za mikutano ya kabla ya mchezo (MCM) yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara na kugharimu klabu nyingi.
Faini ya shilingi milioni tano kwa kila kosa imekuwa kama “gharama ya kawaida” kwa baadhi ya timu, jambo linaloonyesha uzembe katika maandalizi na uendeshaji wa mechi.
Vilevile, baadhi ya klabu zimeadhibiwa kwa kukataa kutumia vyumba rasmi walivyopangiwa, zikiwemo Azam FC, Simba SC na Mashujaa FC, hali inayodhihirisha mgongano kati ya imani binafsi na kanuni za mashindano.
Ikiwa klabu zitachukua hatua za makusudi kuboresha mifumo yao ya uendeshaji, kuwekeza katika taaluma na kudhibiti tabia za mashabiki, basi zinaweza kuepuka hasara hizo la sivyo, nusu ya pili ya msimu itaendelea kushuhudia hadithi ile ile ya makosa yale yale na bili ile ile ya faini ikiendelea kuongezeka.
Kwa upande wa wachezaji wao wamekuwa wakikutana na rungu la kuanzia laki tano hadi milioni milioni mbili, ambapo hadi sasa Gabriel Mwaipola wa Mbeya City ndiye pekee mpaka leo ametozwa faini milioni tano baada ya kumpiga kiwiko Rajabu Mfuko wa Namungo anafuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga ambaye jana alitozwa faini ya milioni nne.
Msimamo wa orodha ya adhabu kwa klabu
1. Simba SC: Sh. 30,000,000
2. Dodoma Jiji FC: Sh. 30,000,000
3. TRA United SC: Sh. 25,500,000
4. Mtibwa Sugar FC: Sh. 25,000,000
5. Young Africans (Yanga): Sh. 20,000,000
6. Coastal Union FC: Sh. 15,000,000
7. Tanzania Prisons FC: Sh. 15,000,000
8. Azam FC: Sh. 10,000,000
9. Namungo FC: Sh. 10,000,000
10. Pamba Jiji FC: Sh. 10,000,000
11. KMC FC: Sh. 6,000,000
12. Singida Black Stars: Sh. 5,500,000
13. Mashujaa FC: Sh. 5,000,000
14. JKT Tanzania FC: Sh. 0
15. Singida BS: Sh. 0
16. Mbeya City FC: Sh. 0
Wachezaji waliopigwa faini
Djigui Diarra = 4,000,000
Gabriel Mwaipola = 5,000,000
Vitalis Mayanga = 1,000,000
Khalid Aucho = 1,000,000
Jonathan Sowah = 1,000,000
Allasane Kante = 1,000,000
Seleman Mwalimu = 1,000,000
Abdi Banda = 1,000,000
Duchu = 1,000,000
Andy Lobuka Bikoko = 500,000
Muhsini Malima = 500,000
Mzamiru Yassin = 500,000