Carrick aanza rasmi kazi Man United
Muktasari:
- Kwa sasa, mashabiki wa Man United wanatarajia kuona kama Carrick ataweza kurejesha mwelekeo wa klabu katika kipindi hiki cha mpito.
Manchester, England. Michael Carrick ameanza rasmi majukumu yake kama kocha wa muda wa Manchester United baada ya kuwasili katika uwanja wa mazoezi wa Carrington leo Jumanne asubuhi, akiongoza benchi la ufundi jipya.
Carrick (44), aliyewahi kuwa kiungo mahiri wa United, alionekana akiwasili kwa gari lake aina ya Land Rover Defender, akianza mipango ya kuinusuru klabu hiyo hadi mwishoni mwa msimu baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim wiki iliyopita.
Kocha huyo wa muda amemteua aliyekuwa msaidizi wa timu ya taifa ya England, Steve Holland, kuwa mkono wake wa kulia. Holland (55) ana uzoefu mkubwa katika soka la juu, akifanya kazi kwa zaidi ya miaka 11 chini ya Gareth Southgate kwenye timu za taifa za England.
Hata hivyo, jina la Holland limewahi kuhusishwa na sakata la beki wa Arsenal, Ben White, aliyeondoka kambini wakati wa Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, jambo lililoaminika kusababishwa na sintofahamu baina yao. Tangu hapo, White hajarejea tena kwenye kikosi cha England.
Mbali na Holland, Carrick amemjumuisha Jonathan Woodgate, ambaye aliwahi kufanya kazi naye Middlesbrough, pamoja na Travis Binnion. Woodgate (45), aliyewahi kuchezea Leeds United na Real Madrid, anakumbukwa pia kwa tukio la vurugu la mwaka 2001 lililomuingiza matatani kisheria alipokuwa mchezaji wa Leeds.
Katika mabadiliko mengine, Jonny Evans amerejea Manchester United wiki chache tu baada ya kuondoka katika wadhifa wa mkuu wa mikopo na maendeleo ya wachezaji. Evans (38), aliyestaafu soka mwishoni mwa msimu uliopita, sasa ni sehemu ya benchi la ufundi la Carrick.
United bado haijatoa tangazo rasmi la uteuzi wa Carrick, lakini chanzo cha klabu kimeeleza kuwa uthibitisho huo uko njiani. Carrick na benchi lake la ufundi wanakabiliwa na mtihani mzito mara moja watakapocheza na wapinzani wao wa jadi, Manchester City, Jumamosi ijayo.
Kwa sasa, mashabiki wa Mashetani Wekundu wanatazama kuona kama Carrick ataweza kurejesha mwelekeo wa klabu katika kipindi hiki cha mpito.