Mbappe amuaga Alonso, visa ni hivi
Muktasari:
- Klabu inamshukuru Xabi Alonso na benchi lake la ufundi kwa kazi na kujitolea kwao, na inawatakia kila la heri katika hatua inayofuata ya maisha yao.”
Madrid, Hispania. Kylian Mbappe amekuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kutoa heshima kwa kocha wake wa zamani, Xabi Alonso, baada ya kufukuzwa kazi jana Jumatatu.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44, aliondolewa chini ya saa 24 baada ya Real Madrid kupigwa mabao 3-2 na wapinzani wao wakubwa Barcelona kwenye fainali ya Kombe la Super la Uhispania lililofanyika Saudi Arabia.
Alonso alikuwa ameanza kukabiliwa na presha kubwa katika wiki za hivi karibuni kufuatia tetesi za kutofautiana na wachezaji wake pamoja na matokeo yasiyoridhisha ya klabu yake, hali iliyowaacha Los Blancos wakiwa nyuma kwa pointi nne dhidi ya Barcelona kileleni mwa LaLiga.
Kuondoka kwa Alonso kulitangazwa kuwa ni kwa “makubaliano ya pande zote”, huku aliyekuwa mchezaji mwenzake Liverpool na Real Madrid, Alvaro Arbeloa, aliyekuwa akiinoa timu ya akiba ya klabu hiyo, akiteuliwa kuchukua nafasi yake.
Muda mfupi baada ya taarifa hiyo kutolewa, Mbappe alivunja ukimya wake kupitia ukurasa wake wa Instagram. Akishiriki picha yake akiwa amemkumbatia Alonso katika kile kilichoonekana kuwa ni uwanja wa Santiago Bernabeu, Mbappe aliandika:
“Imekuwa safari fupi lakini ilikuwa heshima kucheza chini yako na kujifunza kutoka kwako. Asante kwa kuniamini tangu siku ya kwanza.”
Maneno hayo mazuri kutoka kwa Mbappe hayakushangaza wengi, ikizingatiwa kwamba mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango bora chini ya Alonso, akifunga mabao 29 na kutoa asisti tano katika mechi 25 pekee msimu huu.
Hata hivyo, kauli hiyo ilikuja baada ya Mbappe kuonekana kudhoofisha mamlaka ya kocha wake kufuatia kipigo cha Super Cup. Katika video iliyosambaa mitandaoni, Alonso alionekana akiwahimiza Mbappe na wachezaji wengine kwenda kuipa Barcelona heshima ya kupita mstari wa heshima (guard of honour) baada ya ushindi wao.
Mbappe alionekana kupinga wazo hilo, akirusha mikono juu kwa hasira kabla ya kuondoka, huku Alonso akionekana kukubali hali hiyo alipomfuata mchezaji wake nyota. Mbappe baadaye alilaumiwa kwa Real Madrid kushindwa kuwaheshimu wapinzani wao.
Wengi waliona tukio hilo kama muhtasari wa kipindi cha Alonso kama kocha, akipambana mara kwa mara na changamoto kwa mamlaka yake kutoka kwa wachezaji wake mwenyewe. Hali hiyo ilionekana zaidi kwa Vinicius Junior, ambaye aliripotiwa kumwambia rais wa Real Madrid, Florentino Perez, mapema msimu huu kuwa hatasaini mkataba mpya ikiwa Alonso angeendelea kuwa kocha.
BBC Sport, pia iliripoti kuwa Alonso na Mbappe walibishana kuhusu mbinu za mchezo kabla ya pambano la Jumapili. Alonso alikuwa amejiunga na Real Madrid miezi minane tu iliyopita baada ya kipindi chenye mafanikio makubwa akiwa Bayer Leverkusen, ambapo aliipa klabu hiyo taji lao la kwanza kabisa la Bundesliga.
Baada ya kuondoka Leverkusen mwishoni mwa msimu uliopita, Alonso alichukua mikoba jijini Madrid kabla ya Kombe la Dunia la Klabu, mashindano ambayo Real Madrid walitolewa hatua ya nusu fainali. Alishinda mechi 13 kati ya 14 za kwanza za ligi, lakini kipigo cha Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool mapema Novemba kiligeuka kuwa mwanzo wa matatizo, huku Madrid wakishinda mechi mbili pekee kati ya nane zilizofuata.
Tetesi za migawanyiko katika kambi ya mazoezi hazikumsaidia kocha huyo, huku magazeti ya Hispania yakiripoti kuwa hadi wachezaji watano hawakuridhishwa na mbinu zake. Ilielezwa kuwa Thibaut Courtois, Jude Bellingham na Vinicius Junior walikuwa na wasiwasi kuhusu falsafa ya Alonso, hasa msisitizo wake wa kujenga mashambulizi kutoka nyuma.
Vinicius hasa alionekana kutoridhika chini ya utawala wa Alonso na baada ya kutolewa katika mchezo wa El Clasico mwishoni mwa Oktoba, hakuficha hasira zake. Baadaye alitoa radhi hadharani kwa “wachezaji wenzake, klabu na rais”, lakini jina la Alonso halikutajwa.
Nahodha wa klabu, Fede Valverde, naye aliripotiwa kuwa na mashaka kuhusu mbinu za Alonso na alilazimika kukanusha tetesi kwamba alikataa kucheza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Kairat Almaty mwezi Oktoba. Hii ilikuwa baada ya Alonso kumtumia kama beki wa kulia kutokana na kukosekana kwa Trent Alexander-Arnold na Dani Carvajal, huku Valverde akisema kwa msisitizo: “Sikuzaliwa kucheza beki wa kulia.”
Hata hivyo, Alonso alifanikiwa kuleta mabadiliko ya muda mfupi kipindi cha sikukuu, Real Madrid wakishinda michezo mitano mfululizo katika mashindano yote. Lakini kiwango hicho hakikutosha kuwashawishi viongozi wa Bernabeu kuendelea naye, na sasa anatarajiwa kuhusishwa na kurejea Ligi Kuu ya England katika miezi ijayo.
Katika taarifa ya kuondoka kwake, klabu imesema:
“Real Madrid CF inatangaza kuwa, kwa makubaliano ya pande zote kati ya klabu na Xabi Alonso, imeamuliwa kumaliza kipindi chake kama kocha wa kikosi cha kwanza.
Xabi Alonso ataendelea kuwa na upendo na heshima ya mashabiki wote wa Madrid kwa kuwa ni gwiji wa Real Madrid na daima amewakilisha maadili ya klabu yetu. Real Madrid daima itakuwa nyumbani kwake.
Klabu inamshukuru Xabi Alonso na benchi lake la ufundi kwa kazi na kujitolea kwao, na inawatakia kila la heri katika hatua inayofuata ya maisha yao.”
Taarifa nyingine iliyotolewa dakika chache baadaye iliongeza:
“Real Madrid CF inatangaza kuwa Alvaro Arbeloa ndiye kocha mpya wa kikosi cha kwanza.”