Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Casemiro amfuata Chikola Jangwani

Muktasari:

  • Taarifa ya utambulisho wa Casemiro ndani ya Yanga jana ilisema,"Karibu Jangwani Abdulnassir Mohamed. Mdogo kiumri, mpevu kisoka. Casemiro ni Mwananchi."

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kumtambulisha Offen Chikola kama mchezaji wake mpya, Yanga jana imetangaza kumnasa kiungo mkabaji, Abdulnassir Abdallah ‘Casemiro’ kwa mkataba wa miaka mitatu.

Casemiro anajiunga na Yanga baada ya kuonyesha kiwango bora katika kikosi cha Mlandege ambacho kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu uliomalizika wa 2024/2025 huku yeye akiwa miongoni mwa nyota tegemezi.

Taarifa ya utambulisho wa Casemiro ndani ya Yanga jana ilisema,"Karibu Jangwani Abdulnassir Mohamed. Mdogo kiumri, mpevu kisoka. Casemiro ni Mwananchi."

Usajili wa Casemiro unaonekana kulenga kuiongezea Yanga machaguo zaidi katika nafasi ya kiungo wa ulinzi hasa baada ya kuondoka kwa Khalid Aucho ambaye anaripotiwa kuwa katika mpango wa kujiunga na timu mojawapo ya Israel.

Kufuatia kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na Aucho, Yanga iliingia sokoni haraka na kumnasa kiungo Moussa Balla Conte wa CS Sfaxien ya Tunisia na baada ya hapo imetua kwa Casemiro ambaye inaripotiwa kwamba alikuwa pia kwenye rada za Azam FC na Singida Black Stars.

Casemiro anakuwa mchezaji wa nne kutoka Visiwani Zanzibar ndani ya kikosi cha Yanga akiungana na beki Ibrahim Abdulla 'Bacca' na viungo Mudathir Yahya na Shekhan Khamis.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 ni miongoni mwa viungo waliofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita akicheza mechi zote 30 za Mlandege ambayo ilimaliza ikiwa bingwa.

Yanga imeonekana kuvalia njuga dirisha hili kubwa la usajili kutokana na haraka ambayo imekuwa nayo katika kunasa wachezaji inaowahitaji huku pia ikihusishwa kufikia makubaliano na nyota kadhaa ambao inategemea iwe nao kuanzia msimu ujao.

Mbali na Casemiro, Conte na Chikola ambao tayari imeshawatambulisha, Yanga inaripotiwa imeshamalizana na Mohamed Hussein 'Tshabalala', Lamine Kouma na mshambuliaji Andy Boyeli na inahusishwa pia na kuwahitaji Feisal Salum na Edmund John.