Prime
MZEE WA FACT: Balla wa Yanga na mabalaa mengine
Muktasari:
- Picha rasmi ambayo Yanga walianza nayo ilimuonesha nyota huyo akiwa na Rais wa Yanga wakicheza chess huku kete wanazotumia ni za rangi nyekundu...dharau kubwa sana!
Yanga wamemtambulisha Moussa Balla Conte, kiungo wa ulinzi kutoka klabu ya CS Sfaxien ya Tunisia, raia wa Guinea. Hili ni pigo kubwa sana watani wao wa jadi, Simba SC, kwani mchezaji huyo alikuwa kwenye malengo yao na walishaanza mazungumzo naye.
Katika mahojiano ambayo aliyafanya na moja ya vituo vya redio nchini, meneja habari wa Simba SC ndugu Ahmed Ally, alithibitisha kwamba Balla Conte alikuwemo kwenye ripoti ya kocha wao Fadlu Davies na walishaanza mazungumzo naye.
Kabla mazungumzo hayajafika mbali, Yanga wamemtangaza. Tena sio tu kumtangaza, bali kwa kuwakoga Simba SC. Picha rasmi ambayo Yanga walianza nayo ilimuonesha nyota huyo akiwa na Rais wa Yanga wakicheza chess huku kete wanazotumia ni za rangi nyekundu...dharau kubwa sana!
Ilivyokuwa
Ni kweli kwamba Simba walimhitaji sana mchezaji huyo na ni kweli kwamba kocha Fadlu Davies alishaongea naye na uongozi wa Simba ulishakubaliana naye kila kitu. Bahati mbaya kwao waliweka maneno matupu...bila vitendo. Maneno matupu bila pesa ni kelele. Yanga wakawa na kasi zaidi...wakaifuata klabu yake wakamalizana nayo na kuhamia kwa mchezaji...wakaweka maneno kidogo mapesa mengi...game over!
Balla Conte ni muendelezo wa mabalaa ambayo Yanga wamekuwa wakiifanyia Simba kipindi cha usajili kwa miaka kadhaa. Hii ni nje ya kuibiana wachezaji kama ambavyo Inasemekana nahodha wa Simba, Mohamed Hussein Zimbwe Jr. maarufu kama Tshabalala, tayari ameshasaini Yanga. Inasemekana Zimbw alisaini usiku wa Jumatatu ya Julai 14 kuamkia Jumanne ya Julai 15. Injinia Hersi akiwa ofisini kwake na wasaidizi wake, walituma mkataba Misri kwa mchezaji huyo ambaye yupo huko na timu ya taifa. Naye akaupokea, akaudurufu (scan) kisha akasaini na kuutuma tena Dar es Salaam...kazi imeisha.
Tabia kama hii imezoeleka sana kwa panda zote na ndio maana Rais wa awamu ya tano, Jakaya Kikwete, aliwataka Yanga wakubali yaishe kwa Bernard Morrison mwaka 2021, akikumbushia mkasa wa Gilbert Mahinya 'mashine'. Lakini hii tabia ya kupokonyana tonge mdomoni, imekuwa ya upande mmoja zaidi, Yanga wakiifanyia Simba.
1. Mbuyu Twitte 2012
Mwaka 2012 mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Cup, yalifanyika nchini na klabu ya APR ya Rwanda ilikuja na kiraka mmoja wa kuitwa Mbuyu Twitte. Mchezaji huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyechukua uraia wa Rwanda, akawavutia vigogo wa Dar es Salaam. Simba wakaifuata APR kuulizia huduma yake. Mwenyekiti wao wa wakati ule, Ismail Aden Rage, alisafiri hadi Kigali Rwanda, akamalizana na viongozi wa APR ambao ni maafisa wa jeshi la Rwanda, na akapiga picha na mchezaji.
Kumbe walikosea sana. Mbuyu Twitte alikuwa kwa mkopo APR akitokea FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. APR hawakuwa na mamlaka ya kumuuza bila idhini ya klabu yenye mkataba naye. Yanga wakafunga safari hadi Lubumbashi inakopatikana FC Lupopo, wakamalizana nayo. Klabu ikatoa baraka kwa mchezaji...akakubali, akahamia Yanga. Siku anakuja nchini, alishukia terminal two na alitokea geti dogo la nje ili kuepusha msongamano. Katika kuwakoga Simba, Yanga walimvalisha mchezaji huyo jezi namba nne yenye jina la Rage, Mwenyekiti wa Simba aliyepiga naye picha.
2. Ephraim Makoye 2000
Mwaka 2000, Yanga SC ilimsajili kijana wa kidato cha pili shule ya sekondari Makongo, aliyekuwa akiichezea Kagera Stars (sasa Kagera Sugar), aliyeitwa Ephraim Makoye. Baadaye ikabainika kuwa kijana huyo pia alisajiliwa na Simba, hivyo kuzua utata mkubwa. Wakati huo mambo ya mikataba ya wachezaji na vilabu hayakuwepo na wala chama cha soka (FAT) hakikuyatambua kabisa.
Kilichofanyika ni chama chenyewe (FAT) kutoa fomu za usajili na vilabu kuzichukua na kuandika majina ya wachezaji wao watakaokuwa nao msimu husika. Halafu FAT itakaa na kuyapitia hayo majina na kutoa taarifa uthibitisho. Wachezaji waliopitishwa wataandikwa ‘CLEARED’, ambao hawakupitishwa wataandikwa ‘NOT CLEARED’, usajili unafungwa. Jina la Ephraim Makoye lilionekana kwenye fomu za Yanga na Simba, hivyo akawa NOT CLEARED. Kesi ikanguruma na fomu za usajili zilipoangaliwa, ikaonekana ya Yanga ilitangulia kwenda, hivyo Simba wakaonekana wakorofi.
Lakini Simba ndio walikuwa wa kwanza kuongea na mchezaji huyo na kumsainisha mkataba, na wakapeleka mkataba waliosaini na mchezaji huyo ambao ulikuwa na tarehe ya nyuma kuliko hata fomu za usajili za Yanga. Lakini FAT wakaukataa mkataba kuutumia kama kielelezo kwa sababu wakati huo mikataba ilikuwa haitambuliwi. Kama klabu itasaini mkataba na mchezaji, utabaki kuwa wa kwao, lakini FAT haiutambui, na hautumiki kwenye usajili. FAT ikaamuru Makoye aende Yanga kwa sababu ndiyo waoitangulia kumsajili, japo hawakuwa na mkataba naye. Simba waliokuwa na mkataba naye, wakamkosa.
3. Pius Buswita 2017
Mwaka 2000 Pius Buswita akitokea Mbao FC ya Mwanza, alihitajika na Yanga na Simba kwa pamoja. Wote wakaongea naye na wote wakamsainisha mkataba. Ilipobainika kasaini kwenye timu mbili, akashitakiwa kwenye mamlaka. Sakata lake lilipofika kwenye vyombo vya sheria, mchezaji huyo akakiri kufanya kosa hilo kwa nguvu za shetani. Kupitia wakala wake, Medi Mtabora, Buswita alisema kwamba shetani alimpitia ndiyo maana akasaini Simba na Yanga! Baada ya vuta nikuvute, Yanga wakafanikiwa kumpata, Simba wakabaki na mkataba.
4. Maxi Nzengeli 2023
Mwaka 2023 Simba waliwasiliana na klabu ya AS Maniema ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakionesha nia ya kumnasa nyota wa Maxi Mpia Nzengeli. Wakakubaliana kila kitu, na klabu na mchezaji. Lakini kama kilichotokea kwa Balla Conte, wakati Simba wakijipanga, Yanga wakaingiza miguu miwili...wakaongea na Maniema na kuwalipa kabisa fedha yao...wakamalizana na mchezaji haraka haraka...Simba wakabaki na manyoya.
Makamu wa Rais wa AS Maniema, Guy Kapya, akiongea na gazeti hili aliwahi kusema wakati wanatoka Kinshasa wakiwa na mchezaji huyo, walikutana na viongozi wa Simba jijini Nairobi. Wakawaambia wanaenda Dar es Salaam kusiani Yanga, viongozi wa Simba wakataka kupindua dili juu kwa juu...lakini Kapya akakataa. Akasema haikuwa ustaarabu kuwatupa watu waliowatumia tiketi ya ndege baada ya kukubaliana na kufanya malipo. Akawalaumu Simba wenyewe kwa kuchelewa kuchukua hatua japo walishakubaliana. Ukimya wao ndio uliowafanya Maniema kupokea ofa nyingine na kufanya biashara.
5. Deus Kaseke 2015
Baada ya kung'aa na Mbeya City, Simba ilipanga kuwachukua wachezaji wawili wa klabu hiyo, Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi. Wakatumiwa tiketi ya ndege kutoka Mbeya waje Dar es Salaam. Yanga nao kumbe walikuwa wanamhitaji Deus Kaseke. Waliposikia kwamba anakuja, wakatuma mtu wao uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Wachezaji wale walipotua tu, Kaseke akashikwa mkono na kupelekea Jangwani.
Mchezo huu mchafu ulisimamiwa na mwandishi mmoja wa habari ambaye alienda uwanjani pale kama kuwahoji...akamfiskishia Kaseke ujumbe na kutokomea naye. Simba wakaishia kumpata Mwalyanzi pekee...tiketi yao ya ndege ikapotea!