Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 11 ya Tshabalala Simba, siyo mchezo

Muktasari:

  • Wachezaji walioletwa kikosini Simba wanaocheza nafasi yake ya beki wa kushoto ni wengi na wameshindwa kufurukuta.

Dar es Salaam. Wahenga walisema, 'Kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho', ndivyo unavyoweza kusema kwa aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala', ambaye ameamua kuachana na kikosi hicho baada ya kukitumikia kwa miaka 11.

Ni miaka 11 unayoweza kusema ya kibabe kwa nyota huyo aliyejiunga na Simba Juni 23, 2014, akitokea Kagera Sugar, ambapo alisainishwa mkataba huo na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya kikosi hicho marehemu, Zacharia Hans Poppe.

Beki huyo alisaini Simba wakati rais wa nchi akiwa ni Jakaya Mrisho Kikwete, akaja John Joseph Pombe Magufuli, na sasa Samia Suluhu Hassan, ambapo baada ya miaka 11 inadaiwa anakaribia kujiunga kwa watani zao wa jadi Yanga, atayocheza msimu ujao.

Wachezaji walioletwa kikosini Simba wanaocheza nafasi yake ya beki wa kushoto ni wengi na wameshindwa kufurukuta ila tu baadhi yao walikuwa ni, Jamal Mwambeleko aliyesajiliwa na kikosi hicho akiwa na kiwango bora wakati akiitumikia Mbao FC.

Mwambeleko licha ya kiwango bora alichokuwa nacho wakati akiwa na Mbao ya jijini Mwanza ila ujio wake Simba ulikuwa kama kaa la moto kwani alishindwa kupenya kwa 'Tshabalala' na mwishoni aliomba kuondoka na kujiunga zake na Singida United.

Mwingine ni Mghana, Asante Kwasi ambaye naye alionekana huenda akapindua ufalme wa 'Tshabalala' Simba wakati anasajiliwa mwaka 2017 akitokea Lipuli ya Iringa kutokana na ubora wake wa kuzuia na wakati huohuo kuanzisha mashambulizi ya hatari.

Kiukweli, Kwasi alionekana ni mchezaji tishio ingawa naye alijikuta akilewa sifa mapema na mwishoni akashindwa kupigania namba na nyota huyo na baada ya kudumu misimu miwili aliondoka ndani ya kikosi hicho 2019 na kujiunga na klabu ya Hafia ya Guinea.

Maisha yalienda kasi kwa nyota huyo kwani hata huko nchini Guinea alishindwa kuonyesha kiwango kizuri na kujikuta pia akiachwa na kurudi tena Bongo na kujiunga na Kitayosce FC kwa sasa Tabora United wakati inashiriki Ligi ya Championship.

Nyota mwingine aliyeingia kwenye mtego wa 'Tshabalala' ni Gadiel Michael ambaye alijiunga na kikosi cha Simba 2019 akiwa ni chaguo namba moja akitokea Yanga ila mambo yalikuwa magumu kwake na baadaye kuondoka na kujiunga na Singida Fountain Gate.

Kucheza Simba au Yanga na kushindwa kuonyesha kiwango kizuri haina maana huwezi kuonekana kwingine kwani baada ya Gadiel kutua Singida alicheza vizuri sana na kupata shavu la kujiunga na kikosi cha Cape Town Spurs FC cha kule Afrika Kusini.

"Kati ya mabeki wote ambao wamewahi kuletwa Simba na kunisumbua ni Gadiel Michael, alikuwa mchezaji bora na mwenye kiwango cha juu sana, sema tu ulikuja Simba wakati mbaya," aliwahi kusema Tshabalala

Nyota mwingine ni beki, Valentin Nouma raia wa Burkina Faso aliyejiunga na kikosi hicho Julai 2024, akitokea FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo, ambaye pia baada ya kucheza msimu mmoja tu aliondoka kwa lengo la kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Hao ni baadhi tu ya wengi walioushindwa 'mziki wa Tshabalala' pale Simba na kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine ili kuokoa vipaji vyao vilivyokuwa vinazidi kudidimia licha ya klabu mbalimbali walizotoka kuonekana wana ubora mzuri.


Makocha waliomfundisha

Hadi anaondoka, beki huyo amefundishwa na jumla ya makocha 16, ambapo alianza Zdravko Logarusic (2013-2014), Patrick Phiri (2014), Goran Kopunovic (2014-2015), Dylan Kerr (2015-2016) na Jackson Mayanja akiwa ni kocha wa mpito mwaka 2016.

Wengine ni Joseph Omog (2016-2017), Pierre Lechantre (2017-2018), Patrick Aussems (2018-2019), Sven Vandenbroeck (2019-2021), Didier Gomes De Rosa (2021), Zoran Manojlovic (2022), Juma Mgunda (wa mpito) (2022), na Roberto Oliveira 'Robertinho' (2023).

Makocha wengine waliomfundisha nahodha huyo katika miaka yake 11 ya utumishi akiwa na kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Msimbazi ni, Abdelhak Benchikha (2023/2024), Juma Mgunda (2024) na Fadlu Davids anayeiongoza timu hiyo hadi sasa.


Mataji aliyoshinda 

Kombe la Mapinduzi (2015), Kombe la Shirikisho la FA (2017), Ngao ya Jamii (2017), Ligi Kuu Bara (2017/2018), Ngao ya Jamii (2018), Ligi Kuu Bara (2018/2019), Ngao ya Jamii (2019), Ligi Kuu Bara (2019/2020) na Kombe la Shirikisho la FA (2020).

Mataji mengine aliyotwaa nyota huyo ni Ngao ya Jamii (2020), Ligi Kuu Bara (2020/2021) na Kombe la Shirikisho la FA (2021).


Mafanikio kimataifa

Kombe la Shirikisho Afrika (2017-2018)-16 bora, Ligi ya Mabingwa Afrika (2018/2019)-robo fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika (2019/2020)-16 bora, Ligi ya Mabingwa (2020/2021)-robo fainali na Ligi ya Mabingwa Afrika (2021/2022)-16 bora.

Mafanikio mengine ni Kombe la Shirikisho (2021/2022)-robo fainali, Ligi ya Mabingwa 2022/2023)-robo fainali, African Football League (2023)-nusu fainali, Ligi ya Mabingwa (2023/2024)-robo fainali na Kombe la Shirikisho (2024/2025)- hatua ya makundi.

Msimu huu ndio bora zaidi kwa nyota huyo baada ya kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kupita miaka 32, tangu ilipofika mwaka 1993, ambapo ilikosa ubingwa msimu huu mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.


Tuzo binafsi 

Nyota huyu ameshinda tuzo nyingi binafsi katika kipindi chote alichoichezea Simba, ingawa anakumbukwa zaidi msimu wa 2016/2017, aliposhinda mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu Bara, baada ya kucheza mechi zote 30 bila ya kupumzika wakati huo.