Chama aaanza na rekodi hizi Ligi ya Mabingwa

Muktasari:
- Chama ambaye alijiunga na Yanga akitokea kwa watani wao wa Jadi Simba awali alikuwa anaonekana kuwa anaweza asipate nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Yanga kutokana na ubora wa wachezaji waliopo, lakini ameanza kwa kufanya mambo makubwa.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga Clatous Chama ameanza na rekodi akiwa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye kikosi hicho.
Chama aliiongoza Yanga kupata ushindi wa jumla ya mabao 10-0 dhidi ya Vital O, akiwa amehusika kwenye mabao sita, amefunga mawili na kutoa pasi nne za mabao kwenye michezo hiyo miwili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Chama ambaye alijiunga na Yanga akitokea kwa watani wao wa Jadi Simba awali alikuwa anaonekana kuwa anaweza asipate nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Yanga kutokana na ubora wa wachezaji waliopo, lakini ameanza kwa kufanya mambo makubwa.
Mzambia huyo kama ilivyokuwa kwa Simba, ndivyo imekuwa kwa Yanga. Mara zote amekuwa akianza msimu kwa gia ndogo, lakini kadri siku zinavyokwenda ndivyo balaa lake linazidi kuonekana.
Na kwa sasa ameanza kuonyesha rangi zake halisi akiwa Yanga kupitia mechi hizo mbili za CAF ambazo aliisaidia timu hiyo kupata ushindi wa mabao 10-0 na kuwa klabu ya pili kwa mechi za raundi ya awali kufunga mabao mengi nyuma ya Black Bulls ya Msumbiji iliyopo Kombe la Shirikisho iliyoshinda 11-0.
Chama tayari amethibitisha hilo Yanga baada ya kuanza msimu kwa kupooza na kukaa benchi hadi kufikia baadhi ya watu kuzusha habari kuwa Chama hana furaha katika klabu hiyo, kiungo huyo ameanza kuukumbusha umma bado yupo na moto wake ni ule ule.
Juzi Jumamosi amerejea kwenye ubora wake wakati Yanga ikicheza mechi ya marudiano Ligi ya Mabingwa hatua ya awali dhidi ya Vital'O kutoka Burundi na kushinda kwa mabao 6-0.
Chama aliamka. Katika mabao hayo sita yaliyofungwa na Yanga, Mwamba la Lusaka alihusika na mabao matano akifunga moja na kuastisti mara nne katika mchezo huo.
Baada ya mchezo kumalizika, kiungo mwenzake wa Yanga, Mudathir Yahya alipoulizwa kuhusu ubora wa Chama alijibu maneno mawili tu "We hauogopi?"
Jibu hilo ni ishara tosha ya Chama kuwa kwenye ubora wake. Huenda huko mazoezini anaonyesha ubora mkubwa hali ya kuwafanya kina Mudathir na viungo wengine wa timu hiyo 'kuogopa.'
Kitendo cha Chama kuhusika kwenye mabao matano kati ya sita ya Yanga ni muendelezo tu, kwani katika mechi ya awali dhidi ya Vital'O, alihusika katika mabao mawili akifunga moja katika ushindi wa 4-0.
Kwa sasa ni kwamba Chama amehusika na mabao sita kati ya 10 katika mechi mbili tu, kwa nini Mudathir asihoji; 'We hauogopi?'
Mabao mawili aliyoyafunga katika mechi hizo mbili dhidi ya Vital'O yamempaisha Chama zaidi na kuendeleza rekodi zake katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ameendelea kuwa kwenye orodha ya wafungaji bora 10 wa muda wote wa mashindano hayo akifikisha jumla ya mabao 23 na kukaa nafasi ya saba. Anayeongoza hapa ni staa wa zamani wa TP Mazembe ya DR Congo Tresor Mputu aliyefunga mabao 39.
Aidha Chama anakuwa mchezaji aliyewahi anayecheza Ligi Kuu anayeongoza kwa mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabao hayo mawili yamemfanya kumpiku nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyefunga mabao 21 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia Chama ndiye mchezaji Mzambia mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mabao 23 yanamfanya kushikilia rekodi hiyo akiweka gepu la mabao 10 na anayemfuata ambaye ni Reinford Kalaba aliyefunga mabao 13 kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.
WASIKIE WADAU
Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' alisema Chama ni mchezaji wa daraja la juu katika Ligi ya Tanzania na anapaswa kupewa heshima kubwa.
"Chama ni mchezaji mkubwa na anastahili heshima. Ni mchezaji anayefanya mambo makubwa, yasiyowezekana kwake yanawezekana. Muda ambao hautarajii afanye jambo flani yeye analifanya kwa ufasaha hiyo ndio sifa yake kuu," alisema Mwaisabula.
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mrisho Ngassa alisema Chama kujiunga na Yanga ni ushindi tosha kwa klabu hiyo.
"Sasa yupo Yanga na amekuta timu ina viungo wengine bora, hivyo lazima ushindi uwepo lakini pia ni faida kwa benchi la ufundi kwani watakuwa na machaguo mengi. Naamini huo ni mwanzo tu, Chama atafanya makubwa zaidi ndani ya Yanga," alisema Ngassa.
Huyo ndiye Chama aliyetua nchini kwa mara ya kwanza Julai 2018 akijiunga na Simba kutokea Lusaka Dynamos ya kwao Zambia na kudumu hapo hadi mwaka 2021 alivyojiunga na RS Berkane ya Morocco ambako pia hakudumu kwani baada ya miezi sita tu alirejea Simba na kukaa kwa kikosini hapo hadi msimu huu alipojiunga na Yanga.