Chelsea yafikia pazuri kumnasa Garnacho
Muktasari:
- Garnacho ameichezea Man United zaidi ya mechi 95, amefunga mabao 18 na kutoa asisti 14 tangu alipopandishwa timu ya wakubwa mwaka 2022.
Manchester United iko hatua za mwisho kufikia makubaliano ya kumuuza winga wake chipukizi wa kimataifa wa Argentina, Alejandro Garnacho, 21, kwenda Chelsea kwa ada inayokadiriwa kuwa kati ya Pauni 35-40 milioni.
Garnacho ameichezea Man United zaidi ya mechi 95, amefunga mabao 18 na kutoa asisti 14 tangu alipopandishwa timu ya wakubwa mwaka 2022.
Chelsea inamwona kama sehemu ya mipango ya muda mrefu staa huyu ambaye kocha wa Man United, Ruben anaona haendani na mifumo yake.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu uliopita alicheza mechi 58 za michuano yote, akafunga mabao 11 na kutoa asisti 10.
Hadi sasa, Garnacho ameshafanya makubaliano binafsi na Chelsea na kilichokuwa kinakwamisha ni maslahi baina ya timu na timu. Kocha Enzo Maresca anaamini staa huyu anaendana na mifumo yake.
Christopher Nkunku
AC Milan imeingia vitani kutaka kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Christopher Nkunku, 27, ambaye pia anawindwa na mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich pamoja na klabu yake ya zamani RB Leipzig.
Nkunku amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu ajiunge Chelsea kwa ada ya takribani Pauni 52 milioni mwaka 2023. Akiwa na Leipzig alifunga mabap 70 na kutoa asisti 40 katika mechi 172.
Jorgen Strand Larsen
NEWCASTLE inatarajiwa kutuma ofa mpya ya Pauni 60 milioni kwenda Wolves ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Norway, Jorgen Strand Larsen, 25, baada ya kuwasilisha ofa mbili hapo awali ambazo zote zilikataliwa. Larsen alisajiliwa na Wolves msimu uliopita kwa mkopo kabla ya kusainishwa mkataba wa kudumu katika dirisha hili. Msimu uliopita alifunga mabao 14 katika mechi 38 michuano yote.
Gianluigi Donnarumma
KIPA wa PSG, Gianluigi Donnarumma, 26, bado ana matumaini ya kuondoka katika klabu hiyo kabla ya dirisha kufungwa, huku Manchester City ikitajwa kuwa ndio chaguo lake pekee. Hata hivyo, Man City inasubiri kwanza hadi itakapomuuza kipa wake wa kimataifa wa Brazil, Ederson ndio imsajili yeye. Donnarumma ana mkataba wa kuitumikia PSG hadi mwakani lakini kocha Luis Enrique ameamua kutoendelea naye katika kikosi.
Savinho
MANCHESTER City imeiambia Tottenham rasmi kwamba haina mpango wa kumuuza winga wa kimataifa wa Brazil, Savinho, 21, katika dirisha hili hata kama itatoa ofa ya zaidi ya Pauni 60 milioni. Savinho alisajiliwa na Man City kutoka Troyes mwaka jana na msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote, akafunga mabao matatu na kutoa asisti 13. Kocha wa Spurs, Thomas Frank anamhitaji.
John Victor
WEST Ham inataka kumsajili kipa wa kimataifa wa Brazili John Victor, 29, kutoka Botafogo, lakini klabu hiyo inataka dau kubwa zaidi ya Pauni 6 milioni. Victor ambaye amecheza mechi zaidi ya 130 za michuano yote tangu ajiunge na Botafogo mwaka 2019, ameivutia sana West Ham kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu Juni mwaka huu.
Tomas Soucek
MABOSI wa West Ham wameiambia Everton kwamba hawana mpango wa kumuachia kiungo wao Tomas Soucek, 30, baada ya klabu hiyo ya Merseyside kufanya mawasiliano ya awali. Soucek ameichezea West Ham zaidi ya michezo 180 tangu ajiunge 2020 akitokea Slavia Prague na alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichoshinda Europa Conference League 2023.
Nayef Aguerd
SUNDERLAND inataka kuingia katika vita dhidi ya Marseille, AC Milan na AS Roma kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa West Ham na Morocco Nayef Aguerd, 29, katika dirisha hili. Aguerd alisajiliwa na West Ham mwaka 2022 kwa Pauni 30 milioni kutoka Rennes na msimu uliopita alicheza kwa mkopo Real Sociedad. Staa huyu aling’ara akiwa na timu ya taifa ya Morocco katika Kombe la Dunia mwaka 2022.