Chelsea yamnasa mshambuliaji kutoka Brighton

Muktasari:
- Chelsea tayari wamekamilisha usajili wa Liam Delap huku wakiwa kwenye hatua za mwisho za kumnasa Jamie Gittens kutoka Borussia Dortmund.
Klabu ya Chelsea imekamilisha makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa Brighton, Joao Pedro, kwa ada ya paundi milioni 60 (Sh204 bilioni) na hivyo kuimbwaga Newcastle iliyokuwa ikimwania pia nyota huyo mwenye umri wa miaka 23.

Chelsea awali ilituma ofa ya paundi milioni 58 ambayo ilikataliwa na Brighton, lakini imeongeza dau hilo hadi kufikia makubaliano kamili.
Pedro aliripotiwa kuonyesha wazi kuwa anapendelea kujiunga na kikosi cha Enzo Maresca, baada ya mazungumzo na viongozi wa Stamford Bridge.

Pedro kucheza Kombe la Dunia la Klabu
Chelsea wana hadi Julai 3 kuwasilisha majina ya wachezaji wapya kwenye kikosi cha michuano ya kombe hilo, ambapo watacheza dhidi ya Palmeiras mjini Philadelphia, Marekani.
Pedro anatarajiwa kuungana na wenzake nchini humo hivi karibuni baada ya wachezaji kupewa mapumziko ya siku mbili mjini Miami.

Mkataba wa miaka saba unapangwa
Pedro atatolewa mkataba wa muda mrefu wa miaka saba, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Chelsea wa kuwekeza kwa vipaji chipukizi.
Kocha Maresca anavutiwa na uwezo wake wa kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji, pembeni, kama namba 9 au nyuma ya mshambuliaji wa kati.

Muendelezo wa njia ya Brighton
Pedro anakuwa mchezaji mwingine kujiunga na Chelsea kutoka Brighton, baada ya wachezaji kama Marc Cucurella, Moises Caicedo, na Robert Sanchez kufanya hivyo awali. Pia, Levi Colwill alitolewa kwa mkopo Brighton kabla ya kurejea Chelsea.
Mshambuliaji huyu ameichezea Brighton jumla ya mechi 70 katika mashindano yote tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Watford ambapo mpaka sasa ameifungia Brighton mabao 30 na kuchangia pasi tisa za mabao.

Pedro alikosa mechi za mwisho wa msimu wa Brighton baada ya kutokea ugomvi mazoezini na beki Jan Paul van Hecke.
Hata hivyo, Chelsea wameonyesha imani naye, wakiamini anaweza kuleta uhai mpya katika safu ya ushambuliaji.
Chelsea tayari wamekamilisha usajili wa Liam Delap huku wakiwa kwenye hatua za mwisho za kumnasa Jamie Gittens kutoka Borussia Dortmund.