Danny Mrwanda anapiga hela ndefu kwa siku

Wednesday May 25 2022
mrwanda pic
By Imani Makongoro
By Charity James

DANNY Mrwanda anaamini Yanga inakufa Jumamosi hii mbele ya Mnyama Jijini Mwanza kwenye nusu fainali ya Kombe la ASFC.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam, Mrwanda ambaye msimu huu aliichezea Ken Gold ya mkoani Mbeya amezungumza mambo kibao ya kuvutia. “Kwenye dabi bahati tu, japo naweza kuipa Simba kwa kuwa sioni kama wanaweza kukubali wakose vyote, hapa kwenye dabi timu itakayokuwa na bahati siku hiyo ndiyo itashinda, ila kwenye ligi Yanga ina nafasi kubwa ya ubingwa ukiangalia pointi zake, morali na mechi ilizobakisha.”


340,000 KWA SIKU

Jijini Dar es Salaam kama umewahi kupanda au kushuhudia daladala zimeandikwa Mrwanda, huo ni miongoni mwa miradi inayomuingizia pesa mwanasoka huyo wa zamani wa Yanga na Simba.

“Hesabu kwa baadhi ya daladala hizo ni Sh 80,000 mpaka 100,000 kwa siku, nilikuwa nazo tisa lakini sasa zimebaki nne,” anasema Mrwanda.

Advertisement

Kwa daladala ambazo anamiliki, Mrwanda anaingiza Sh 340,000 kwa siku, japo pia anafanya biashara ya spea za magari jijini Dar es Salaam na mkoani Mbeya kuna biashara ambazo anazifanya.

“Japo sio kikubwa lakini alichonijalia mwenyezi Mungu kinanisaidia, kuna biashara nyingi nyingi nafanya, kuna watu wanasimamia, ili hata nikistaafu ziendelee vizuri,” ambaye ni baba wa watoto watatu.


DEREVA AKIZINGUA UNAKAA MWENYEWE

Kila biashara ina changamoto zake ikiwamo ya daladala ambayo Mrwanda anasema ikitokea mmoja wa madereva wake amezingua, haoni tabu kuchukua jukumu hilo.

“Japo siku hizi hakuna usumbufu huo kama zamani, utaratibu umebadilika kwa sasa anayepewa mkataba ni dereva na anapokuja kuamsha gari ananipa hesabu kabisa asubuhi ndipo anachukua gari.

“Yeye akienda kulaza gari, asifanye kazi ipasavyo hiyo ni juu yake, kwani tayari hesabu ya siku anakuwa ameshatoa, mimi ninachompa mtaji wa mafuta, ambayo siku akirudisha gari anarudisha na mafuta uliyompa, hii kwa asilimia kubwa imesaidia kuondoa purukushani,” anasema.


SOKA LA NJE

“Nakumbuka nikiwa Kuwait, Marekani ilipokuwa ikiishambulia Iraq wakati Saddam Hussein akiwa madarakani, iliweka ngome yake Kuwait, muda wote ndege za kivita zilikuwa zinakatisha kwenda kuishambulia Iraq,” anasema Danny Mrwanda.

“Nilikutana na mazingira ya vita maeneo tofauti, sio Kuwait pekee, hata Vietnam nilipokwenda kucheza kule hakukuwa salama sana, lakini mwanaume ukienda kutafuta maisha ile ni kama ajali kazini, ndivyo ilikuwa kwangu,”.


UJASIRIAMALI ULIANZA HIVI

Licha ya mazingira ya nchi ya Vietnam kuwa na matukio kadhaa ya vita, Mrwanda anasema ni sehemu ambayo aliyafurahi maisha ya soka katika historia yake ya mpira.

Anasema nchi hiyo ilimthamini na kuthamini mchango wake uwanjani, watu wa nchi hiyo walimpa thamani inayostahili katika safari yake ya soka la kulipwa.

“Nimecheza Kuwait, Rwanda na Sweden, lakini sehemu ambayo nilifurahia kucheza soka la kulipwa ni Vietnam, sababu ina watu ambao ukifanya kazi vizuri wanakuthamini.

“Nimekwenda kule nikiwa kwenye ubora wangu, kiwango changu kilikuwa juu, nikawa nafanya kazi bora ndani ya uwanja na kuwapa matokeo mazuri, nje ya uwanja wao pia walinithamini sana,” anasema.


KILA KLABU INA NDEGE

Anasema wakati akicheza soka la kulipwa nchini humo, kila timu ambayo ilikuwa kwenye Ligi yao ilikuwa ina uwezo kifedha.

“Klabu zote zilikuwa zinamiliki ndege zao binafsi na viwanja, tena sio viwanja vidogo vya mazoezi, uwanja wa kawaida ulikuwa ni kama uwanja wetu wa Uhuru.

“Ni nchi ambayo ilikuwa imejiwekeza kwenye soka, hata usajili wa klabu hizo ulikuwa ni mkubwa, walikuwa wakisajili wachezaji hadi kutoka Brazil,” anasema.

Anasema nchini humo aliyafurahia maisha ya soka, lakini pia alipata pesa kidogo ambazo ziliweza kumsaidia kwenye maisha yake na kumpa mafanikio kadhaa.

“Mkataba wangu wa kwanza ulikuwa wa mwaka mmoja, walinipa dola 120,000(Sh279Milioni), na mshahara wa dola 14,000(Sh32Milioni) kwa mwezi, mkataba wa miaka miwili walinipa dola 240,000(ShSh558Milioni). Kulikuwa na bonasi, timu ikishinda ya dola 1000(Sh2.3Milioni) kwa mchezaji, lakini pia tukitoka sare kuna bonasi yake, nilicheza kwa mafanikio nchini humo kwa miaka mitano,” anasema.

Anasema kuna baadhi ya wachezaji aliowaacha nchini humo baada ya kustaafu soka waligoma kuondoka kutokana na mazingira rafiki ya soka ambayo walikutana nayo.

“Mimi niliondoka kutokana na mazingira yangu, hapa nyumbani na familia na watoto, siwezi kuwahamisha, hivyo nisingeweza maisha yangu yawe kule halafu wao wabaki Tanzania,” anasema.


MIAKA 20 YA SOKA

Mrwanda ni miongoni mwa wanasoka nchi waliodumu kwenye ushindani wa soka kwa muda mrefu, tangu mwaka 2001.

“Mwaka wa 20 sasa niko kwenye soka, hii ni kwa kuwa ratiba yangu ni nyepesi, kikubwa ni kufuata misingi ya soka, nikitoka kufanya mazoezi lazima nipate muda mrefu wa kupumzika.

“Sina purukushani nyingi baada ya mazoezi,” anasema Mrwanda ambaye baadhi ya watoto wake wameonyesha nia ya kurithi kipaji chake.

“Mke wangu na watoto huwa wananitia moyo, wananitakia heri nikienda kucheza a nikifanya vibaya uwa wananifariji, maombi yao yamekuwa upande wangu, wananipa ushirikiano mkubwa kwenye kipaji changu cha soka, ndio sababu nimedumu kwa muda mrefu.”

Mrwanda alikutana na mkewe shuleni, walikuwa majirani na marafiki wakati huo Mrwanda akiwa kidato cha nne na mkewe kidato cha kwanza, urafiki wao ulidumu hadi walipokuja kufunga ndoa miaka kadhaa baada ya wote kuhitimu masomo.


TUHUMA ZA HUJUMA ZAMUONDOA SIMBA

Safari ya Mrwanda kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Rwanda zilichangizwa na tuhuma za kuhujumu timu kwenye mechi na Yanga.

“Mechi ile ilifanyika Morogoro, Simba tulishinda kwa penalti ila yangu nilikosa.”

Unajua nini kilitokea hapa? Aliona nini? Usikose nakala yako kesho.


Advertisement