De Bruyne amtaka Grealish Napol
Muktasari:
- Guardiola, amenukuliwa akimwambia wazi Grealish kuwa ni wakati wa kuondoka ili kutafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Naples, Italia. Nyota mpya wa Napoli, Kevin De Bruyne, anaripotiwa kumshauri kocha mpya wa timu hiyo, Antonio Conte, kumsajili winga wa Manchester City Jack Grealish, ambaye kwa sasa hana uhakika wa mustakabali wake Etihad.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na klabu hiyo ya Serie A, De Bruyne ambaye amejiunga na mabingwa hao wa zamani wa Italia katika dirisha hili la majira ya joto, anaamini kuwa Grealish anaweza kuwa silaha muhimu kwenye mfumo wa Conte ikiwa ataletwa Naples.
Grealish, 29, alijiunga na Manchester City mwaka 2021 akitokea Aston Villa kwa dau la pauni milioni 100 (takriban Shilingi bilioni 330 za Kitanzania), na kuweka rekodi kama mchezaji wa Kiingereza ghali zaidi wakati huo. Hata hivyo, licha ya kung’ara katika msimu wa 2022/23 ulioshuhudia City wakitwaa Treble (Premier League, FA Cup na Champions League), Grealish ameshindwa kuonyesha makali yake kwa kiwango cha kudumu tangu kuwasili Etihad.
Katika msimu wa 2024/25, hali ya Grealish ilizidi kuwa mbaya, akianza mechi saba pekee za Ligi Kuu na moja tu mwaka 2025. Hatimaye, aliondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 27 wa Manchester City kilichosafiri kushiriki Kombe la Dunia la Klabu, hatua iliyozua maswali mengi kuhusu hatima yake.
Kocha Pep Guardiola amethibitisha kuwa walikubaliana na Grealish kwamba ni vyema aondoke kutafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara. "Jack ni mchezaji wa kipekee, lakini kwa sasa anahitaji kucheza kila baada ya siku tatu ili kurudisha kiwango chake cha zamani. Bila yeye, msimu wa Treble usingekuwa rahisi. Hivyo, kwa manufaa ya pande zote, ni bora aondoke," amesema Guardiola.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Conte amekuwa akizungumza kwa kina na De Bruyne kuhusu Grealish, akiomba maoni ya kiufundi kuhusu uwezo na hali ya sasa ya nyota huyo. De Bruyne, ambaye ana ushawishi mkubwa kutokana na hadhi yake kwenye soka la kimataifa, anatarajia Napoli watachukua hatua na kufanya usajili huo kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Iwapo dili hilo litafanikiwa, Grealish atajiunga na mastaa wengine waliowahi kucheza Ligi Kuu ya England waliopo Napoli kama Scott McTominay, Billy Gilmour, Romelu Lukaku, na Philip Billing, ambao walikuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hiyo msimu uliopita.
Kwa sasa, Manchester City wako tayari kupokea ofa ya mkopo endapo hakuna timu itakayoweza kukubali kumnunua moja kwa moja, huku mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki sawa na Sh990 milioni ukiwa changamoto kwa baadhi ya klabu. Everton ni miongoni mwa vilabu vinavyohusishwa na nyota huyo, ambaye anataka kurejea kwenye kiwango chake ili awe sehemu ya kikosi cha Thomas Tuchel kitakachoshiriki Kombe la Dunia la 2026.
Endapo atahamia Napoli, Grealish atakuwa anaanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka, akiwa na nia ya kurejesha heshima na kiwango kilichomfanya awe mchezaji ghali zaidi England. Na kwa Conte, ushawishi wa De Bruyne unaweza kuwa kichocheo muhimu cha kujenga upya ushindani katika Ligi ya Seria A.