Diallo aibeba United, akipiga hat trick

Muktasari:
- Baada ya kufunga mabao hayo Diallo anakuwa mchezaji wa tatu katika historia ya Ligi Kuu England ya kufunga mabao matatu ndani ya dakika 10 za mwisho
Manchester,England. Winga wa Manchester United, Amad Diallo ameisaidia timu yake kupata ushindi baada ya kuifungia mabao matatu hat trick katika mchezo wa Ligi Kuu Engaland dhidi ya Southampton iliopigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Man United ilitoka nyuma kwa bao moja alilojifunga Manuel Ugarte dakika ya 43, ambalo lilidumu mpaka dakika ya 82 baada ya Amad Diallo ambaye alianza kwa kuisawazishia United.
Diallo alifunga tena bao la pili dakika ya 90 akiunganisha pasi ya Christian Eriksen kabla ya kufunga bao la tatu dakika 90+4, ambapo aliupokonya mpira kutoka kwa beki wa Southampton uliokuwa umepigwa na kipa wake Aaron Ramsdale.
Baada ya kufunga mabao hayo Diallo anakuwa mchezaji wa tatu katika historia ya Ligi Kuu England ya kufunga mabao matatu ndani ya dakika 10 za mwisho baada ya kufanya hivyo Ole Gunnar Solskjaer dhidi ya Nottingham Forest Februari 1999 na Wayne Rooney dhidi ya Hull City, Januari 2010.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim baada ya mchezo kumalizika amesema: “Diallo amekuwa na msimu mzuri sana, hongera kwake natumaini atafurahia usiku wa leo kwa sababu amefanya jambo zuri, lakini tunapaswa kuwa waangalifu na vijana wadogo kwani mchezo huu umeshapita."
Nyota huyu amecheza jumla ya mechi 12, akiwa amefunga mabao nane. Alianza kucheza baada ya kuondoka kwa Erik ten Hag ambaye alikuwa akimuacha benchi lakini Ruud van Nistelrooy ambaye alikuwa kocha wa muda alimuamini na kuanza kumpa nafasi ambayo anaipata mpaka sasa kwa Ruben Amorim.
Manchester United inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 26 katika mechi 21 ilizocheza wakati Southampton yenyewe inaburuza mkia ikiwa na pointi sita.
Mchezo ujao Manchester United itakuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Brighton, Januari 19, 2025