Dilunga kurudi uwanjani Januari

KIUNGO Hassan Dilunga ameamua kuvunja ukimya baada ya kutokea sintofahamu ya kutotambulishwa katika Tamasha la Simba Day.

Gazeti mama la Mwananchi liliwahi kumkariri Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu akisema Dilunga bado ni mchezaji wao na yupo kwenye matibabu, ingwa si kati ya waliotangazwa kuachwa au kuagwa rasmi kama ilivyokuwa kwa Tadeo Lwanga, Cris Mugalu na Meddie Kagere.

Mwananchi lilimtafuta Dilunga na alisema mkataba wake umeisha (Umebakiza siku chache) na bado hajasaini mkataba mpya na timu hiyo lakini bosi (Jina kapuni) alisema atamtafuta.

“Upande wa afya yangu naendelea vizuri lakini kurudi uwanjani ni Januari Mungu akipenda,” alisema Dilunga ambaye aliumia goti na kushindwa kumalizia msimu na alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu.

Wachezaji wa zamani katika kikosi hicho wameonyesha kutokukubaliana na kitendo cha Simba kutotoa taarifa rasmi juu ya mchezaji huyo.

Zamoyoni Mogela alisema “Kwa mazingira haya maana yake hakuna mawasiliano, mchezaji ni majeruhi kwa hiyo kama wanaachana inabidi watangaze kuliko kuja kumuacha kienyeji.”

Upande wa Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema ;”Kama taarifa haitoki basi kuna shida sehemu, mtu hawezi kuachwa kienyeji na wanapokaa kimya inakuwa ngumu lakini Simba ni lazima itoe taarifa kuhusu Dilunga.”