Dolly Parton aimba 'chanjo chanjo' baada ya kuchanjwa

Thursday March 04 2021
dolly pic

Washington, Marekani (AFP)
Kutoka "Jolene" hadi "Vaccine (chanjo)" -- gwiji wa muziki wa country, Dolly Parton amepata chanjo ya kwanza na kushauri Wamarekani kufuata mfano wake, akiimba kibao chake cha zamani cha kusifia chanjo.
"Chanjo, chanjo, chanjo, nawaomba tafadhali, msisite," aliiamba akitumia sauti ya wimbo wake uliotamba wa mwaka 1973. "Chanjo, chanjo chanjo, kwa sababu ukifa, inakuwa ushachelewa," yanasema mashairi ya wimbo huo.
Katika video fupi iliyotumwa katika mitandao ya kijamii, mwimbaji huyo mwenye miaka 75 anaonekana akichomwa Moderna, chanjo ambayo alitoa fedha kusaidia kuitengeneza. 
"Nina umri mkubwa wa kutosha kuipata (chanjo) na ni makini kuipata.... ninataka kumwambia kila mtu kwamba nadhani ni lazima utoke na kuipata," alisema. 
Akiheshimiwa na watu wa kada tofauti kwa miongo kadhaa, Parton, ambaye ni mfadhili wa muda mrefu, amekuwa akitokea katika habari za hivi karibuni, hasa baada ya kutoa msaada wa dola 1 milioni za Kimarekani (sawa na Sh2.3 bilioni za Kitanzania) kwa Chuo Kikuu cha Vanderbilt.
Fedha hizo zilienda kusaidia kutengeneza chanjo ya Moderna dhidi ya virusi vya corona.
Parton ameungana na watu maarufu wengine wa Marekani ambao wamesema hadharani kuwa wamesaidia chanjo hiyo kama wacheza filamu Tom Hanks na Sean Penn.

Advertisement