Doumbia atimka CHAN, aiwahi Yanga Dar

Beki mpya wa Yanga Mamadou Doumbia, amechukua maamuzi magumu ya kuikacha kambi ya timu ya Taifa Mali inayoshiriki mashindano ya CHAN yanayoendelea nchini Algeria kisha akawaaambia uongozi anakwenda kujiunga na kambi ya klabu yake mpya.
Doumbia ni kati ya mastaa wa kigeni waliosajiliwa na Yanga katika dirisha dogo lililofungwa Jumapili usiku Januari 15, akija kuongeza nguvu katika ukuta wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara.
Juzi mashabiki wa Yanga wakati timu yao inacheza na Ihefu walikuwa na maswali mengi jukwaani wakihoji staa huyo atatua nchini lini, lakini sasa jibu limepatikana.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Doumbia alisema ameamua kuja haraka kujiunga na timu yake mpya akiwa na imani na mastaa wanaowaacha katika timu ya taifa lake.
Mali ilicheza mchezo wake wa kwanza juzi Januari 16 dhidi ya Mauritania na kutoka sare ya mabao 3-3, huku Doumbia akikosekana katika mchezo huo.
"Jambo zuri ni klabu zote zimeelewana na shirikisho la Mali pia, nimeona niwahi haraka kujiunga na timu yangu mpya, nasubiria tiketi ya ndege ili nije Tanzania (juzi) alisema Doumbia.
Beki huyo mrefu aliongeza kuwa amefurahi kukiamilika kwa dili hilo ambapo anajipanga kuja kuwa na maisha mapya kusaka mafanikio sawa na kipa na raia mwenzake wa Mali Djigui Diarra.
"Nimefurahi kujiunga na Yanga hii ni klabu kubwa lakini nina ndugu zangu hapo Diarra na Kanoute (Sadio wa Simba), nafurahia kuona mafanikio yao tangu wamekuja hapo nahitaji kupita njia kama hiyo."