DR Congo kuumana na hawa mchujo Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mechi za hatua ya mwisho ya mchujo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitachezwa Machi 2026 zikihusisha timu sita kutoka mabara matano tofauti duniani.
Wapinzani watano wa DR Congo katika mechi za hatua ya mwisho za mchujo kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 wamejulikana rasmi usiku wa kuamkia leo baada ya mechi za mwisho za hatua ya kawaida ya kuwania kufuzu mashindano hayo kukamilika rasmi.
Mechi hizo za hatua ya mwisho ya mchujo ambayo itahusisha timu za mabara matano tofauti zimepangwa kuchezwa Machi mwakani ambapo timu hizo sita zitasaka tiketi mbili za kucheza Kombe la Dunia.
DR Congo ambayo itacheza ikiwakilisha bara la Afrika, wapinzani wake kutoka Kanda ya soka inayowakilisha Bara la Amerika Kaskazini na Kati (CONCACAF) ni Jamaica na Suriname.
Suriname imemaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi A la kanda ya CONCACAF lililoongzwa na Panama iliyofuzu wakati huo Jamaica yenyewe imeingia mchujo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi C la kanda yake nyuma ya vinara Curacao.
Kutoka Kanda ya CONMEBOL ambayo inawakilisha nchi za Bara la Amerika Kusini, timu iliyoingia hatua ya mwisho ya mchujo ni Bolivia.
Mshindani mwingine wa DR Congo ni New Caledonia, timu inayotokea katika Kanda ya Soka ya Oceania na Kanda ya Asia, timu itakayocheza mchujo ni Iraq.
DR Congo ilifanikiwa kutinga hatua ya mwisho ya mchujo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya Penalti 3-2 dhidi ya Nigeria katika mechi ya fainali ya kuwania tiketi hiyo kupitia bara la Afrika.
Katika hatua ya nusu Fainali, DR Congo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Cameroon.
fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.