Eze afichua siri ya kutua Arsenal
Muktasari:
- Mkali huyo wa England, Eze, 27, alitambulishwa uwanjani Emirates Jumamosi iliyopita kabla ya Arsenal kuichapa Leeds United 5-0 baada ya kukamilisha uhamisho wa Pauni 67.5 milioni kutokea Crystal Palace.
LONDON, ENGLAND: Nyota mpya wa Arsenal, Eberechi Eze amefichua ni kama alikuwa kwenye majaribio ya kikosi hicho kwa miaka minne akijaribu kuwashawishi asajiliwe mara zote alizocheza dhidi yao.
Mkali huyo wa England, Eze, 27, alitambulishwa uwanjani Emirates Jumamosi iliyopita kabla ya Arsenal kuichapa Leeds United 5-0 baada ya kukamilisha uhamisho wa Pauni 67.5 milioni kutokea Crystal Palace.
Eze ambaye amekuwa shabiki wa Arsenal tangu utoto wake aligomea ofa ya kwenda kujiunga na Tottenham Hotspur baada ya Mikel Arteta kuvamia dili hilo na kumtaka akacheze kwenye chama lake huko Emirates.
Eze alimwaga machozi wakati alipoachwa na akademia ya timu ya Arsenal huko Hale End, wakati alipokuwa na umri wa miaka 13 na tangu wakati huo amekuwa akicheza kwa nguvu zote mara zote alizocheza dhidi ya wababe hao wa Emirates.
Aliichezea Crystal Palace uwanjani Emirates dhidi ya Arsenal mara nne katika kipindi chake cha miaka mitano aliyokuwa Selhurst Park, alifunga katika mechi ya mwisho alipokwenda uwanjani hapo kwenye sare ya 2-2, Aprili mwaka huu.
Eze alisema: “Nimekuwa kwenye majaribio kwa miaka minne kwa kusema ukweli. Mara zote nilizokuja Arsenal, nilikuwa nakiangalia kitu nilichokuwa nakikalia wakati nilipokuwa nakuja kutazama mechi na ndugu zangu.
“Nimekuwa nikisema kila wakati: ‘Ni hivi, ni wakati na hii ni fursa.’ Sisemi nilikuwa nafahamu hiki kitakwenda kutokea, lakini nilikuwa na hisia hiyo. Nilikuwa nawaza juu ya kurudi hapa.”
Eze anajiandaa kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England Arsenal itakapokwenda Anfield kukipiga na Liverpool, mechi ambayo inatoa mapema taswira ya mbio za ubingwa.
Kuhusu mafanikio anayotaka kuyafikia huko Arsenal, Eze alisema: “Ninachotaka ni kushinda, nataka kushinda kila kilichopo mbele. Nimeanza kupata hisia ya jambo hilo, nitachangia na kujitolea kwa nguvu zote kusaidia timu kushinda. Hilo ndilo lililopo kwenye akili yangu.”