Fainali Kombe la Shirikisho kupigwa Babati
Muktasari:
- Msimu uliopita, fainali ya mashindano hayo ilichezwa katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza kuwa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu itachezwa katika Uwanja wa Tanzanite, Babati.
Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa uamuzi huo umechukuliwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo baada ya kuona kuwa uwanja huo unakidhi vigezo vya kuandaa mchezo huo.
"Tunapeleka mashindano haya kutoa shukrani na sapoti kwa juhudi ambazo zinafanywa na maeneo husika na kuendeleza mpira huko. Kuna baadhi ya mikoa tumeipa changamoto hiyo, warekebishe miundombinu ili tuweze kuwapa nafasi hiyo," alisema Karia.
Karia alisema kuwa kabla ya hatua hiyo ya fainali, kutakuwa na mechi za hatua ya nusu fainali ambazo mojawapo itachezwa Mwanza.
"Uwanja ambao utachezwa nusu fainali nyingine bado hatujatangaza. Kuna mikoa ambayo tumeipa changamoto ya kuboresha miundombinu na utakaokidhi vigezo tutaupa fursa hiyo," alisema Karia.
Ikumbukwe kwamba katika msimu uliopita, fainali ya mashindano hayo ilichezwa katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Yanga iliibuka bingwa baada ya kuifunga Azam FC kwa bao 1-0