Ferguson alivyozima ndoto ya Young kucheza na mwanae
Muktasari:
- Ashley Young alionekana kusubili mechi hii kwa hamu baada ya droo iliyochezeshwa kuonyesha Everton inakutana na timu hiyo anayochezea mwanae lakini hakujua kuwa asingeweza kutimiza ndoto yake baada ya mchezo huo kumalizika.
Liverpool, England. Kocha wa Peterborough United, Darren Ferguson amezima ndoto ya mchezaji wa Everton, Ashley Young ambaye alikuwa na matumaini ya kucheza pamoja na mwanae, Tyler Young (18) kwenye uwanja wa Goodison Park katika mashindano ya FA ambapo Everton ilikuwa nyumbani dhidi ya Peterborough.
Historia inaonyesha kuwa hakuna hata mwaka mmoja ambao baba na mwana waliwahi kucheza kwenye kiwanja kimoja tangu kuanzishwa kwa mashindano haya ambapo ilikuwa inategemewa kutokea jana lakini hilo lilishindikana baada ya kocha wa Peterborough, Darren Ferguson ambaye ni mtoto wa Sir Alex Ferguson kutompanga Tyler Young.
Ashley Young (39) aliingia kwenye mchezo huo akitokea benchi dakika ya 73 wakati timu yake ikiongoza bao 1-0 huku mwanae, Tyler Young akiendelea kukaa benchi hadi dakika 90 zinamalizika ambapo Everton iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Baada ya mchezo huo, Darren Ferguson alieleza sababu za kumuacha mchezaji huyo, akisema kuwa hawezi kuendesha mchezo kwa hisia.
“Haikuwa rahisi kumwacha Tyler benchi, lakini nilihitaji kufanya kilicho bora zaidi kwenye timu, tungekuwa tunaongoza 2-0 wakati huo, ningemweka Tyler, lakini tulikuwa nyuma 1-0, hivyo niliamua kumuingiza mshambuliaji. Hatuwezi kuonekana kama tunaendesha mchezo kwa hisani,” alisema Ferguson.
Kwa upande wa Ashley Young hakuonyeshwa kufurahishwa na maamuzi ya kocha huyo huku akiandika ujumbe kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) akionyesha hisia za huzuni baada ya kuandika neno "GUTTED" lenye maana ya kuumizwa na kile kilichotokea jana.
Ashley Young ni mmoja kati ya mastaa wenye historia kubwa katika soka la England akicheza kwa mafanikio zaidi akiwa na Manchester United kabla ya kwenda Inter Milan, kisha Astona Villa na sasa Everton. Pia alikuwa sehemu ya timu ya England iliyofika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018.
Wakati Ashley Young akishindwa kutimiza ndoto ya kucheza na mwanaye wapo nyota wengine waliowahi kufanya hivyo katika historia ya soka.
Mwaka 2014 katika kikosi cha Mogi Mirim huko Brazil, Rivaldo akiwa na miaka 41, alicheza sambamba na mwanawe, Rivaldinho aliyekuwa na miaka 18.
Wengine ni George Eastham Sr na George Eastham Jr (Ards FC mwaka 1954), wakati Alexei Eremenko Sr akifanikiwa kucheza na wanawe wawili, ambao ni Alexei Eremenko Jr katika kikosi cha HJK Helsinki mwaka 2003, pamoja na Roman Eremenko mwaka 2004 katika kikosi cha FF Jaro.