Gamondi awapa onyo kali mastaa Yanga

Muktasari:
- Yanga itakuwa ugenini mbele ya Warundi hao kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 1:00 jioni ya kesho kabla ya kurudiana nao wikiendi ya wiki ijayo Kwa Mkapa na mshindi wa pambano hilo atasonga mbele kuvaana na mshindi wa mchezo kati ya SC Villa ya Uganda au CBE ya Ethiopia
Dar es Saalam. Zikiwa zimebaki saa chache, kabla ya Yanga kushuka uwanjani kuvaana na Vital'O ya Burundi katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wa kikosi hicho, Miguel Gamondi awachimba biti mastaa wa timu hiyo ili isije ikawakuta aibu mbele ya wapinzani wao hao.
Yanga itakuwa ugenini mbele ya Warundi hao kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 1:00 jioni ya kesho kabla ya kurudiana nao wikiendi ya wiki ijayo Kwa Mkapa na mshindi wa pambano hilo atasonga mbele kuvaana na mshindi wa mchezo kati ya SC Villa ya Uganda au CBE ya Ethiopia.
Akizungumza na Mwananchi, jana Gamondi amesema, mastaa wa timu hiyo wamekuwa na kiwango bora katika mechi chache walizocheza, ila hawatakiwi kujiamini kuwa watashinda mchezo ujao.
Aidha alieleza kuwa, aliwaambia hivyo kwani mpinzani wao ni mpya kabisa kwao hivyo wasiwachukulie poa, jambo ambalo halitakiwi katika mpira wa miguu.
“Vital'O ni timu ambayo hatujawahi kucheza nayo hivi karibuni, hivyo wachezaji hawatakiwi kujiamini na matokeo ya mechi zilizopita," alisema Gamondi na kuongeza;
"Kuwafunga Simba na Azam sio kigezo cha wao kujiamini kupitiliza kuwa na hawa Waburundi watafunga ila nidhamu ya hali ya juu ndio inayotakiwa. Mashindano haya ni tofauti na ligi hivyo huwezi kupima kiwango cha mpinzani wako kwa namna yoyote kwani lolote linaweza kutokea.”
Gamondi anaingia katika mechi hiyo ya kesho akiwa na rekodi ya kuishia robo fainali ya msimu uliopita ikitolewa kwa penalti na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini ikitoka kutwaa Ngao ya Jamii ikianza kwa kuifunga Simba bao 1-0 kisha kuizamisha Azam kwa mabao 4-1 katika mechi kali ya fainali.