Gomes aikomoa Yanga

Muktasari:
KOCHA Didier Gomes mjanja sana. Amepitia video ya mchezo wa kwanza dhidi na Yanga na kubaini Nasreddin Nabi alimzidi wapi na fasta akaamua kupanga jeshi lake kwa kuwapa mapumziko mafupi baada ya mechi ya jana ya Ligi Kuu kabla ya kuwahi mapema Kigoma.
KOCHA Didier Gomes mjanja sana. Amepitia video ya mchezo wa kwanza dhidi na Yanga na kubaini Nasreddin Nabi alimzidi wapi na fasta akaamua kupanga jeshi lake kwa kuwapa mapumziko mafupi baada ya mechi ya jana ya Ligi Kuu kabla ya kuwahi mapema Kigoma.
Simba na Yanga zinavaana katika fainali ya Kombe la ASFC itakayopigwa Jumapili ijayo mjini Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na Gomes ameapa iwe isiwe ni lazima washinde ili kulipa kisasi kwa Nabi, pia kuipa timu taji la pili msimu huu baada ya lile la Ligi Kuu wanalokabidhiwa leo.
Gomes alisema kwa kutambua umuhimu wa mchezo wa Kigoma utakaopigwa saa 9:00 alasiri, atawapa mapumziko ya siku mbili vijana wake, kisha Jumatano watalihama Jiji la Dar kuwahi Kigoma, saa 24 kabla watani wao kufika huko na kuanza mikakati ya kumaliza mapema mechi ya fainali.
Kocha huyo alipoteza mechi ya kwanza katika Ligi Kuu akiwa na Simba kwa kufungwa na Yanga, Julai 3 na alisema amepitia video ya mechi na kubaini wapi alijikwaa na analipanga jeshi lake kuhakikisha wanarejesha heshima yao kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Alifichua moja ya dawa ya kuizima Yanga ni kutumia washambuliaji watatu kama alivyofanya dhidi ya Azam waliowatangulia kwa bao la Idd Seleman ‘Nado’ kabla ya kuwavuruga kwa kumuingiza Chris Mugalu aliyeungana na John Bocco na Meddie Kagere na kurudisha bao.
Washambuliaji hao watatu wamefunga mabao 40, kitu alichosema anaamini ndio watakaoimaliza Yanga Kigoma, akisema hata hivyo ataanza na wawili kwanza kupima upepo na hali ikiwa ovyo atamuingiza mwingine kuifanyizia Yanga kama ilivyokuwa majuzi dhidi ya Azam.
Gomes alisema katika mechi hiyo ataanza na mastraika wawili kati ya Bocco, Mugalu na Kagere na mmoja wao atakuwa benchi, na uwezo wao mkubwa wa kufunga anaamini watalitimiza hilo.
“Unajua kuwatumia Bocco, Mugalu na Kagere kwa pamoja maana yake ni mwendo wa kushambulia na kutaka kupata bao, juzi dhidi ya Azam ilisaidia kupata matokeo mazuri, baada ya awali kukwama katika ligi tulicheza na Yanga,” alisema.
“Moja ya silaha tutakayoitumia ni hii ya mastraika hao watatu kwa pamoja dhidi ya Yanga, tunataka kubeba ubingwa wa ASFC na kumaliza msimu kwa heshima kubwa baada ya kutetea Ligi Kuu.”
Gomes alikiri licha ya kikosi chake kuwa bora, lakini walipata upinzani kwenye Ligi na hata ASFC dhidi ya Yanga na Azam kwa kushinda mechi moja, sare tatu na kupoteza moja, kitu asichotaka kitokee Kigoma.
Alisema wamekutana na Azam mara tatu msimu huu, wametoka sare mbili katika ligi na kuwafunga nusu fainali ya ASFC, huku Yanga ikicheza nao mara mbili na kupata sare na kipigo kimoja.
“Binafsi pamoja na wachezaji wangu tunakwenda kujipanga ili nasi tupate matokeo ya ushindi dhidi ya Yanga msimu huu, kwani tutasherehekea ushindi wa derby na kutwaa ubingwa wa ASFC,” alisema.
SAA 24 MBELE
Katika kuhakikisha wanatimiza lengo, Gomes ameutaka uongozi timu iondoke saa 24 kabla ya watani wao ili kupata muda wa kujiaandaa vyema Kigoma.
Mratibu wa Simba, Abbas Ali, alisema baada ya mchezo na Namungo watapumzika siku mbili kabla ya Julai 21 kuwahi Kigoma.
Simba itaondoka ikiwa ni saa 24 kabla ya Yanga kuwafuata kwani imepanga kutua Kigoma Julai 22 baada ya kumalizana leo na Dodoma Jiji katika Ligi Kuu.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema baada ya mchezo kikosi kitarudi Dar kufanya maandalizi ya mwisho kwa siku tatu kisha kitaenda Kigoma.