HansPope afariki dunia

Muktasari:

  • Hans Poppe hadi umauti unamfika alikuwa bado yupo Hospitali alikopumzishwa kwa takribani wiki mbili.

Taarifa mbaya kwa medani ya michezo ni kwamba aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba Zacharia HansPope amefariki dunia.

HansPope amefikwa na umauti usiku huu katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa amepumzishwa kwa zaidi ya wiki mbili.

Klabu ya Simba kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram umethibitisha taarifa hizo za kifo cha kiongozi huyo ambaye amewahi kushikilia nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya wekundu hao kwa kipindi kirefu.

Inaelezwa kwamba hali ya HansPope ilibadilika ghafla ndani ya siku tatu na kumpelekea kufariki leo usiku.

Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Simba Salim Abdallah 'Try Again amesema siku tatu nyuma HansPope alikuwa anaendelea vyema kiasi cha kuchat katika makundi mbalimbali ya WhatsApp hali ambayo iliwapa imani kwamba wakati wowote ataruhusiwa kutoka hospitali.

"Hali yake ilibadilika ghafla ndani ya siku tatu kutoka leo lakini kabla ya hapo bodi nzima tulijua kwamba angeruhusiwa alikuwa akijadiliana mambo mbalimbali kwenye makundi yetu ya WhatsApp, hili la usiku huu sio tu limetushtua ila limetuumiza sana," amesema Try again

HansPope atakumbukwa kwa misimamo yake mikali ndani na nje ya Simba lakini pia  kuwa mstari wa mbele kuipigania Simba kwa fedha na mambo mbalimbali hatua ambayo ilimjengea heshima kubwa