Prime
Hizi hapa sababu Mwenda kusajiliwa Yanga

Muktasari:
- Tuanze na fundi huyo wa eneo la Aucho ambaye kukosekana kwake kwenye mechi kadhaa, pengo lake limeonekana kwa Yanga kupasuka baadhi ya mechi, kitu kilichoufanya uongozi wa klabu hiyo kuingia sokoni fasta ili kushusha vifaa vipya vya kuziba pengo pale anapokosekana.
Mabosi wa Yanga wameamua, baada ya jana kumtambulisha beki wa pembeni, Israel Mwenda na Mwanaspoti linakudadavulia kwa nini klabu hiyo imemnyakua beki huyo aliyeibuka mazoezini pamoja na kikosi cha sasa, lakini kuna fundi mwingine wa mpira yupo njiani kutua eneo analocheza Khalid Aucho.
Tuanze na fundi huyo wa eneo la Aucho ambaye kukosekana kwake kwenye mechi kadhaa, pengo lake limeonekana kwa Yanga kupasuka baadhi ya mechi, kitu kilichoufanya uongozi wa klabu hiyo kuingia sokoni fasta ili kushusha vifaa vipya vya kuziba pengo pale anapokosekana.
Inaelezwa majeraha ya mara kwa mara sambamba na umri alionao Aucho yamewafanya viongozi wa klabu hiyo kufanya maandalizi ya maisha mapya bila yeye, ndiyo maana tayari fasta wameanza kumpiga hesabu Kelvin Nashon, huku wakimtolea macho kiungo mkabaji wa FC Lupopo.
Mabosi wa Yanga wamefanya mazungumzo ya kumbeba Nashon kwa mkopo kutoka Singida Black Stars na wamenasa jina la kiungo mkabaji wa kigeni wa FC Lupopo ya DR Congo, Mick Harvy Itali Ossété (25).
Inaelezwa wapo hatua za mwisho za kumchukua Nashoni kwa mkataba wa miezi sita, lakini wanataka kumvuta Ossete mwenye uraia wa Congo Brazzaville kwa aina ya uchezaji wake eneo hilo la kati.
Mwanaspoti, linafahamu Nashon tayari yupo jijini Dar es Salaam muda wotote anaweza kutambulishwa na Yanga, huku mabosi wa klabu hiyo wakifanya mazungumzo na Ossete.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga, kimeliambia Mwanaspoti ni kweli wana Aucho na amefanya makubwa ndani ya timu hiyo, lakini wanapambana kunasa saini ya Ossete ili kuiweka timu katika nafasi ya kutumika bila presha.
“Aucho amecheza misimu mitatu mfululizo kwa ubora mkubwa na ndio chaguo la kwanza la kila benchi hii ni kutokana na kukosa mtu wa kumpa changamoto tunapambana kuhakikisha tunapata kiungo mwingine mkabaji wa kigeni ambaye atatupa kitu sahihi,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Suala la nani kumpisha mwingine sio muhimu sana kulizungumzia sasa mchezaji bora na ambaye ataipa timu kile tunachokitaka ndiyo atakuwa sahihi kuendelea kuitumikia Yanga inayohitaji ushindani wa wachezaji kwenye kila namba wakiwa na uwezo sawa.”
Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema jina la kiungo huyo wa Lupopo anayetajwa pia kuwindwa na Singida BS, lilipofika kwa Kocha Sead Ramovic, aliwataka mabosi hao watulie kwanza akiwataka wamtangulize Nashon ili kupunguza presha kikosini na kwa hiyo ya Mkongo huyo wasubiri kwanza ajiridhishe naye.
“Inasubiriwa maamuzi ya kocha kama ataridhika naye atatua klabuni, lakini ikishindikana tutaendelea kusaka wengine, ila kwa Nashon kila kitu kimeshakaa sawa atakuja kwa mkopo wa miezi sita,” kilieleza chanzo hicho, huku rafiki wa karibu wa Ossete aliliambia Mwanaspoti taarifa aliyonayo ya awali ni kiungo huyo ana ofa mbili mezani kutoka Singida Black Stars na Yanga.
“Ni mchezaji mzuri anaitumikia timu ya taifa ya Congo Brazzaville, licha ya kucheza chini ana uwezo wa kupanda kutengeneza nafasi na hata kufunga,” alisema rafiki wa karibu wa mchezaji huyo.
Kama Ossete na Nashon watatua Yanga, basi kuna nafasi ya viungo waliopo sasa katika timu hiyo kuonyeshwa mlango wa kutokea ikiwamo kutolewa kwa mkopo.
Nafasi hiyo kwa sasa mbali na Aucho pia ina Duke Abuya, Jonas Mkude, Aziz Andambwile anayemudu pia kucheza kama beki wa kati pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mudathir Yahya wanaomudu kucheza pia kiungo cha ushambuliaji.
USAJILI WA MWENDA
Mapema jana asubuhi, Yanga ilimtambulisha Israel Patrick Mwenda ambaye muda mchache aliibukia katika mazoezi ya timu hiyo, huku wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo wakitofautiana juu ya usajili huo, wakiona kama hawezi kuwa na maajabu mbele ya Yao Kouassi na Chadrack Boka wanatumika beki za pembeni.
Sio Boka na Yao, lakini Mwenda anaenda kuungana na Kibwana Shomary na Nickson Kibabage ambao ni wazi mmojawao ni lazima watampisha beki huyo wa zamani wa Simba na Singida BS.
Mijadala imekuwa mikubwa juu ya utambulisho wa Mwenda, lakini Mwanaspoti katika fukunyua yake imenasa taarifa za kwanini mabosi wa klabu hiyo wameamua kumnasa beki huyo wa zamani wa Alliance FC.
Mashabiki wanajiuliza mtandaoni, Yanga imeona nini kwa beki huyo na je atapindua meza baada ya kuchemsha kwa Shomary Kapombe alipokuwa Msimbazi kiasi cha wawili hao kuchuniana na kuugawa uongozi wa klabu hiyo ya nani aondoka na nani abaki katika dirisha lililopita kabla ya kuibukia Singida BS.
Taarifa hizo zinabainisha kwamba, Mwenda alikuwa kwenye hesabu za Yanga Yanga tangu usajili wa dirisha kubwa msimu huu, lakini dili hilo likafa kutokana na kuwa na mkataba na Simba na iliposikia ameibukia Singida waliona ni nafasi rahisi kwao kumbeba na ndivyo kilichotokea na kutambulishwa rasmi jana.
Sababu ya Yanga kumtaka beki huyo ni uwezo wa kucheza beki ya kulia na kushoto na hata eneo la wingi ndiyo maana ilikuwa ikimpigia hesabu kwa muda mrefu.
NAFASI YAKE
Usajili wa Mwenda unakuwa ni wa kwanza chini ya Kocha Ramovic aliyetambulishwa Novemba 15 mwaka huu akichukua nafasi ya Miguel Gamondi.
Mwenda kutua kwake Yanga inamaanisha sasa timu hiyo itakuwa imepata beki kiraka anayemudu kucheza beki wa kulia na kushoto, pia mwenye uwezo wa kucheza winga na kumrahisishia kazi Ramovic kumchezesha katika mfumo wa 3-5-2 unaotumia zaidi mabeki watatu nyuma.
Katika mfumo wa 3-5-2, mabeki wa pembeni (wing-backs) wana jukumu muhimu na la kipekee. Mfumo huu unajumuisha mabeki watatu (center-backs) na wachezaji watano katikati ya uwanja na mabeki wa pembeni wanakuwa sehemu muhimu ya kuunganisha ulinzi na mashambulizi.
Kwa kifupi, mabeki wa pembeni katika mfumo wa 3-5-2 wanachukua majukumu ya kuungana na timu ya ulinzi na mashambulizi kwa nyakati tofauti. Wakati timu inashambulia wanapaswa kwenda kuongeza nguvu, lakini mashambulizi yakirudi kwao hawana budi kurudi kwa wakati kukaa kwenye maeneo yao kuzuia hatari.
VITA IPO HAPA
Ujio wa Mwenda utamuweka katika wakati mgumu beki wa kulia, Kibwana Shomari aliyeonekana kushindwa kupenya mbele ya Yao, lakini hata kwa Kibabage anayecheza beki ya kushoto naye atakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kusalia kikiosini kwani bado amekuwa akiwekwa benchi na Boka aliyesajiliwa dirisha kubwa.
ENZI ZA SINGIDA
Mwenda akiwa Singida, hakuwa na wakati mzuri kwani nafasi ya beki wa kulia alikutana na changamoto ya namba mbele ya Ande Koffi Cirille raia wa Ivory Coast.
Pia upande wa kushoto anapoweza kucheza kuna mtu makini, Ibrahim Imoro, hivyo kuifanya nafasi yake kuwa finyu chini ya Kocha Patrick Aussems aliyetimuliwa Novemba 29 aliyekuwa akimtumia katika mechi kadhaa.
SIMBA JE?
Mwenda alikwama kudumu Simba kutokana na uwepo wa Kapombe ambaye ndiye alikuwa chaguo la kwanza kwa kipindi cha misimu mitatu aliyocheza kikosini hapo akitokea KMC, huku kukiwa pia na David Kameta ‘Duchu’ anayemudu pia kucheza kulia na kushoto kama beki huyo mpya wa Yanga.
Licha ya kwamba hakuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini kila alipopewa nafasi alionyesha uwezo mkubwa kama ule uliomfanya Simba imasajili kutoka Alliance.
Kama hujui ni Mwenda mwenye miaka 24, alikuwa miongoni mwa nyota waliounda kikosi cha timu ya taifa ya vijana U17, Serengeti Boys kilichoshiriki Fainali za Mataifa Afrika U17 zilizofanyika Gabon mwaka 2017, sambamba na Kibwana Shomari, Nickson Kibabage na nahodha msaidizi Dickson Job.
AANZA MAZOEZI
Taarifa kutoka Yanga zimefichua kwamba, saa chache baada ya kumtambulisha Mwenda kikosini hapo, haraka alianza mazoezi na wenzake yaliyofanyika jana Jumatano asubuhi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Yanga inajiandaa na mchezo wa tatu wa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii nchini humo.