Ishu ya majeraha Azam iko hivi

Katika toleo la Oktoba 16, 2023 la gazeti hili, ukurasa huu ulikuwa na taarifa yenye kichwa cha habari,

AZAM FC IUTAZAME NA UPANDE HUU

Upande ambao tulitaka Azam wautazame ni ule wa idara ya tiba za wachezaji na udhibiti wa majeraha.

Habari ile ilitoka wakati ligi ikiwa katika mzunguko wa tano na Azam FC ilikuwa na wachezaji wanne wenye majeraha.

Abdallah Kheri Sebo ambaye alitarajiwa kuwa nje kwa zaidi ya miezi mitatu, baada ya kuumia kwenye mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.

Yahya Zaydi ambayo alitarajiwa kuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kuumia kwenye mchezo wa tatu wa ligi dhidi ya Singida Big Stars.

Prince Dube ambaye alitarajiwa kukaa nje kwa hadi wiki tatu baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Singida Big Stars. Hata hivyo, alirejea mapema.

Yannick Bangala ambaye hadi wakati huo ilikuwa haijajulikana atakuwa nje kwa muda gani, aliyeumia katika mchezo wa nne dhidi ya Dodoma Jiji.

Huu ulikuwa mwanzo mbaya zaidi kwa Azam FC katika historia ya majeraha klabuni hapo.

Tuliwakumbusha Azam FC kwamba msimu uliopita klabu hiyo ilikuwa na majeruhi mmoja tu aliyekuwa na matatizo makubwa, Malickou Ndoye, ambaye alipatwa na majeraha ya ACL ambayo ni mabaya zaidi kwa wachezaji.

Zaidi ya yeye, ni Abdul Sopu tu ndiye aliyemkaribia, japo naye haikuwa sana!

Lakini msimu huu hadi raundi ya tano, kuwa na majeruhi wanne, iliashiria picha mbaya.

Azam FC ingeweza kuchukua tahadhari juu baada ya onyo lile, lakini nadhani walifumba macho.

Macho waliyofumba wakati ule sasa yanawatesa wenyewe na hali ya majeruhi klabuni imekuwa kubwa kipita maelezo.

Hadi sasa Azam FC ina wachezaji

Ali Ahmada - nje tangu Novemba, 2023

Abdallah Heri - nje tangu Septemba, 2023

Cheikh Sidibe - nje tangu Februari, 2024

Malickou Ndoye - nje tangu Oktoba, 2023

Daniel Amoah - nje tangu Februari 2024

Yanıck Bangala - nje tangu Machi, 2024

Sospeter Bajana - nje tangu Novemba 2023

“Prince Dube” - nje tangu Februari 2024

Alassane Diao - nje tangu Februari 2024

“Abdullah Idrissu” - nje tangu Oktoba 2023

Franklin Navarro - nje tangu Februari 2024

Msimu huu Azam FC ilisajili wachezaji 26 tu, kwa hiyo kukosekana kwa wachezaji 11 maana yake kikosi kinabaki na wachezaji 15 tu.

Hawa ndiyo wachezaji ambao Azam FC ilikuwa nao kuelekea mchezo dhidi ya Yanga, Machi 17.

Na katika hao, wawili walichomwa sindano za kuzuia maumivu ili wacheze, Cheikh Sidibe na Yannick Bangala.

İli kukidhi takwa la kikanuni la kuwa na jumla ya wachezaji 20 kwenye kikosi kamili cha mechi, Azam FC ikaongeza wachezaji watano kutoka timu ya vijana.

Kwa hiyo katika kikosi cha wachezaji 11 walioanza, ni wanne tu ndiyo walikuwa na mbadala kwenye benchi kutoka wachezaji wa timu kubwa.

Wengine walikuwa na mbadala kutoka timu ya vijana, ambao hawana uzoefu wa ligi kuu, halafu dhidi ya Yanga ya akina Pacome na Aziz Ki…masihara hayo.

Kikosi kilipotoka kilionesha Yannick Bangala anaanza, lakini akatolewa sekunde chache kabla ya mechi kuanza na nafasi yake kuchukuliwa na Edward Charles Manyama.

Bangala alishindwa kucheza kwani licha ya kuchoma sindano, bado maumivu aliyasikia.

Kwa hiyo Azam FC ilikuwa na wachezaji sita ambao hawakuwa na mbadala wao kwenye benchi.

Edward Manyama - namba 4

Yeison Fuentes - namba 5

Yahya Zayd - namba 6

Adolf Mtasingwa - namba 8

Feisal Salum - namba 10

Kipre Junior - namba 9

Mmoja wapo kati ya hawa angeumia, basi mbadala wake angekuwa kijana fulani wa kutoka timu ya chini ya miaka 20.

Hadi sasa Azam FC imebakı na mechi 9 za ligi kuu na zingine kadhaa za Azam Sports endapo watakwenda mbali.

Hatua ya ligi iliyobaki ndiyo ngumu zaidi kwani sasa ni kupigania maisha kwa kila timu, aidha ubingwa au kushuka daraja.

Hii maana yake kutakuwa na matumizi mengi ya nguvu na kusababisha majeraha zaidi.

Tunarudia tena, Azam FC inangalie na upande huu