Joshua anarudi baada ya miezi 14
Muktasari:
- Imethibitishwa kuwa pambano kati ya Joshua na Paul litakuwa la kitaaluma, katika uzito wa juu, chini ya sheria za Queensberry si pambano la maonesho. Pia pambano hilo litaonyeshwa moja kwa moja katika Netflix, licha ya Joshua kuwa na mkataba wa muda mrefu na DAZN, ambao umeripotiwa kulipwa fidia kubwa kuruhusu hilo litokee.
Miami, Marekani Pambano kubwa la uzani wa juu kati ya Anthony Joshua na Jake Paul litachezwa mwezi ujao jijini Miami, Marekani, imebainishwa rasmi.
Kwa mujibu wa Daily Mail Sport, pambano hilo linalotarajiwa kufanyika Desemba 19 katika ukumbi wa Kaseya Center litakuwa la kitita cha pauni 140 milioni, ambacho kitapangwa kwa usawa kati ya bingwa wa zamani wa dunia mara mbili, Joshua, na nyota wa mtandao mwenye umri wa miaka 28, Jake Paul.
Pambano hilo litakuwa la raundi nane, kila raundi ikiwa na dakika tatu na mabondia watatumia glavu za uzito wa 10oz. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Joshua, mwenye miaka 36, kurudi ulingoni tangu alipochapwa vibaya na Daniel Dubois miezi 14 iliyopita.
Aidha, kutahitajika mabadiliko makubwa ya uzito wa mabondia hao, kwani kikomo kimewekwa kuwa pauni 245. Joshua amekuwa akipima zaidi ya pauni 250 katika mapambano yake matano ya mwisho, huku Paul akiwa na takribani pauni 200 katika pambano lake la mwisho Juni. Katibu Mkuu wa Bodi ya Udhibiti wa Ngumi Uingereza tayari ametangaza kuwa pambano kama hili lisingepata kibali nchini humo.
Joshua alisema:
"Jake au mtu mwingine yeyote anaweza kupata kazi hii. Hakuna huruma. Nimerudi na nguvu mpya. Najua si kila mtu atanipenda, lakini niko hapa kuvunja rekodi na kufanya mapambano makubwa. Andikeni maneno yangu, huu ni mwanzo tu, nitaivunja mitandao juu ya uso wa Jake Paul."
Kwa upande mwingine, Jake Paulanayejulikana kama "The Problem Child" mwenye rekodi ya ushindi 12 na kupoteza 1, alitamba kuwa “jitu la Uingereza litakuwa usingizini.”
Paul alisema:
"Hii si simulizi ya AI, ni siku ya hukumu. Nikimshinda Anthony Joshua, hakuna atakayebaki na shaka. Naomba radhi kwa watu wa Uingereza, lakini tarehe 19 Desemba, chini ya mwanga wa Miami, fursa inapita na Joshua analala chali."
Hata hivyo, Robert Smith wa Bodi ya Ngumi Uingereza alisema hajafurahi kuona pambano hili limepewa kibali:
"Sioni sababu ya AJ kukubali hili. Hatujapokea ombi lolote na itashangaza sana kama inanishangaza sana kama litafanyika."
Paul alishinda kwa utata dhidi ya Mike Tyson mwenye miaka 58 Novemba mwaka jana, na alimpiga Julio Cesar Chavez Jr kwa pointi. Kupoteza kwake pekee kulitokea dhidi ya Tommy Fury Machi 2024. Kwanza alipaswa kupigana na Gervonta 'Tank' Davis Novemba 14, lakini pambano hilo lilifutwa baada ya Davis kukamatwa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo unyanyasaji na utekaji.
Baada ya pambano la Joshua kuthibitishwa, promota Eddie Hearn alisema:
"Wanasema uwe mwangalifu na unachotamani nahisi ndivyo ninavyotakiwa kusema. Majina mawili makubwa yataumana Desemba 19. Ingawa namheshimu Jake kwa ujasiri, atajifunza njia ngumu Miami."
Imethibitishwa kuwa pambano kati ya Joshua na Paul litakuwa la kitaaluma, katika uzito wa juu, chini ya sheria za Queensberry si pambano la maonesho. Pia pambano hilo litaonyeshwa moja kwa moja katika Netflix, licha ya Joshua kuwa na mkataba wa muda mrefu na DAZN, ambao umeripotiwa kulipwa fidia kubwa kuruhusu hilo litokee.