Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usyk aendeleza ubabe amtaka Fury

Muktasari:

  • Kwa kifupi, pambano hili halikuwa tu ushindi wa Usyk, bali ni pambano la hadhi ya juu ya mchezo wa ngumi na somo kwa wote waliokuwa wakitilia shaka ubora wa bondia huyu kutoka Ukraine.

London, England. Oleksandr Usyk ameonesha kwa mara nyingine kuwa yeye ni bingwa wa kizazi hiki katika mchezo wa ngumi, akimzidi kila idara Daniel Dubois katika pambano lililofanyika juzi usiku katika Uwanja wa Wembley, London.

 Kwa kutumia ujuzi wa hali ya juu, kasi ya ajabu, na akili ulingoni, Usyk alimchapa Dubois raundi baada ya raundi kabla ya kumpiga knockout katika raundi ya tano.

Mashabiki 90,000 walishuhudia jinsi Dubois alivyokuwa hana la kufanya mbele ya mbabe huyo kutoka Ukraine.

 Kuanzia sekunde ya kwanza, Usyk alionekana kuwa daraja tofauti akimchapa Dubois makonde mfululizo, huku akizuia kwa ustadi mkubwa moto.

Katika raundi nne za mwanzo, Dubois hakuwa kupiga ngumi yoyote ya maana, alionekana kuchanganyikiwa, hakuwa na mpango, na kuangaika tu ulingoni.

Katika raundi ya tano, Usyk alimshushia Dubois makonde mfululizo ambapo alimpiga ngumi mbili za mkono wa kushoto na moja ya kulia, zilizomwangusha kwa mara ya kwanza mpinzani wake.

 Aliposimama kwa tabu, Usyk alimaliza kazi kwa mashambulizi ya nguvu na hakukuwa na haja ya kuendelea mwamuzi alimaliza pambano kwa kuhesabu hadi kumi. Dubois alikuwa ameisha na mashabiki walishangilia.

Kama ilivyotarajiwa, Usyk alipokelewa kwa heshima kubwa na mashabiki wa ngumi kutoka kila pembe, hata mbele ya Dubois ambaye ni mzaliwa wa London, lakini alionekana kuwa mgeni.

Wakati wengi walitarajia kuwa Dubois, mwenye miaka 27, angeliweza kulipiza kisasi baada ya kupoteza kwa Usyk miaka miwili iliyopita, pambano hili lilithibitisha kuwa pengo la daraja kati ya wawili hao ni kubwa sana.

Usyk alitumia muda mfupi baada ya ushindi wake kumtaja Tyson Fury kwa pambano la tatu kati yao, pamoja na Derek Chisora na Joseph Parker kuwa wanaotarajiwa kumkabili siku za usoni.

 Akiwa na miaka 38, bado anaonesha kiu ya ushindani akisema: “Miaka 38 si mingi. Nawapenda Wembley, na nitarudi.”

Kwa upande wa Dubois, hatakiwi kuona aibu kupoteza dhidi ya gwiji wa mchezo kama Usyk. Atahitaji kurudi chini, kujijenga upya, na kurudi tena kwa nguvu zaidi.

Kwa kifupi, pambano hili halikuwa tu ushindi wa Usyk, bali ni pambano la hadhi ya juu ya mchezo wa ngumi na somo kwa wote waliokuwa wakitilia shaka ubora wa bondia huyu kutoka Ukraine.