Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamati, hukumu doa Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Ligi Kuu imemalizika Jumamosi kwa Yanga kutwaa ubingwa kwa idadi ya mabao ya kufunga.

Dar es Salaam. Achana na Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu juzi wakiwatimulia vumbi mahasimu wao, Simba na kuwaacha na sintofahamu, habari mpya ni namna mabosi wa zamani wa mpira walivyoichambua Ligi Kuu na ubingwa wa Yanga.

Yanga imetwaa ubingwa huo na kujihakikishia kuendelea kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi 68, sawa na Simba wakitofautina idadi ya mabao.

Yanga imemaliza Ligi ikiwa na mabao 57 ya kufunga na 14 ya kufungwa na Simba mabao 50 ya kufunga na 17 ya kufungwa.

Hata hivyo, Simba nayo inaweza kupunguza machungu ya kukosa ubingwa wa ligi, lakini kupata wa FA na kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika iwapo itaifunga Mbao katika fainali Mei 27.

Simba, ambayo bado haijakubaliana na ubingwa wa Yanga, itaondoka Dar es Salaam mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi kwenda Dodoma kucheza fainali ya FA, lakini ikisisitiza kutorudi nyuma katika harakati za kusaka pointi tatu za mezani kutoka Fifa.

Wakati hayo yakiendelea, aliyekuwa Mwenyekiti wa FAT sasa TFF, Muhidin Ndolanga na Katibu wa zamani wa shirikisho hilo, Fredrick Mwakalebela wameichambua ligi hiyo iliyomalizika juzi.

Mwakalebela alisema kulikuwa na ugumu katika Ligi Kuu Bara ulikuwa wa kiwango cha juu msimu huu na jinsi ligi ilivyomalizika inathibitisha hilo.

“Ligi ilikuwa ngumu, ushindani huo ndiyo unaotakiwa kwani tumeona hata bingwa amesubiri hadi mechi ya mwisho, vivyo hivyo kwa timu za kushuka daraja kuacha JKT Ruvu ambayo ilishuka mapema,” alisema Mwakalebela na kuendelea.

“Msimu huu, Simba, Yanga na Azam hazikuwa na uhakika wa kushinda kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kujihakikishia ushindi hata kabla ya mechi, pale zilipocheza na timu ambazo hazina uwekezaji mkubwa kifedha na Azam kuambulia nafasi ya nne.

“Kikwazo kikubwa msimu huu kilikuwa na uamuzi tata wa kamati za TFF, lakini pia kushindwa kuamua baadhi ya kesi ambazo hadi Ligi Kuu imekwisha hazijafanyiwa kazi, hiyo ni kasoro ambayo binafsi naona ndiyo imevuruga,” alisema Mwakalebela.

Ndolanga hakutofautina na Mwakalebela kuhusu ushindani, lakini akabainisha kwamba endapo timu ndogo zitafanya usajili bora na utawala mzuri kuna uwezekano zikafanya vizuri msimu ujao.

Alisema timu zilizopanda zimeonyesha ukomavu na kulazimisha matokeo katika michezo yao, jambo ambalo limekuwa na msisimko.

“Tumeshuhudia timu kama Mbao, Mtibwa na Kagera zimefanya vizuri msimu huu, maana yake ni kwamba timu kongwe za Simba na Yanga na hata Azam zijipange sana msimu ujao vinginevyo mambo yatakuwa magumu kwao,” alisema Ndolanga.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alisema kuyumba kwa uamuzi kwa baadhi ya kamati kumetia doa.

“Nadhani tatizo kubwa lililosumbua msimu huu ni uamuzi, ambao ulionekana kuyumba. Suala la Simba ndilo limekuwa gumzo kubwa kutokana na jinsi waendeshaji Ligi Kuu walivyolishughulikia.

“Kanuni ziko wazi na hakuna haja ya kuumauma maneno. Wanaofanya maamuzi wawe jasiri na wasioogopa wala kupendelea timu au mchezaji yeyote kwa sababu yoyote ile.

“Vikao vya kikanuni vinatakiwa vifanyike kwa mujibu wa kanuni kuondoa hali iliyozingira suala la Simba na Mtibwa,” alisema.