Kigogo Simba kutua Angola

KATIKA kuonyesha uzoefu na umakini wao kwenye michuano ya kimataifa, Simba tayari ina vichwa Angola kujiweka sawa na mechi yao dhidi ya Clube de Agosto itakayochezwa huko wikiendi ijayo.

Uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ wanataka kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na wanakwepa mizengwe kama waliyofanyiwa Namungo msimu uliopita kwenye Shirikisho ambapo hata mechi yenyewe haikuchezwa.

Mwanaspoti linajua na limejiridhisha kwamba katikati ya wiki hii kigogo mmoja wa Simba, mwenye ushawishi mkubwa klabuni hapo alitangulizwa kuweka mambo sawa akisaidiana na watu wa ubalozi. Kazi yake kubwa ni kuandaa hoteli, usafiri na kuhakikisha mambo yote yanakaa sawa timu ikitua wikiendi ijayo inakwenda moja kwa moja kwenye utaratibu unaoeleweka na wa kisasa.

Wakati hayo mambo ya msingi yakiendelea kuwekwa sawa nchini Angola huku nchini kikosi cha Simba kilirejea jana asubuhi kutoka Zanzibar walipokuwa huko kucheza michezo miwili ya kirafiki.

Kikosi cha Simba kitaondoka nchini Oktoba 8 kuelekea Angola kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza ambao utapigwa Oktoba 9.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema timu yake imepata kipimo kizuri katika michezo miwili waliyocheza hapo Zanzibar na walipata muda wa kutosha kufanya maandalizi kama vile ambavyo walikuwa wanahitaji.

Mgunda alisema walikuwa wanahitaji kupata maandalizi ya kutosha ili kuendelea kuijenga timu yao kiufundi wakati huu ligi ikiwa imesimama kutokana na uwepo wa ratiba ya timu za taifa.

“Akili na nguvu zetu sasa tumeziweka katika michezo ya kimashindano tukianza na ule wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji ambao tutacheza Jumapili tunahitaji kufanya vizuri na kupata ushindi ili kutengeneza morali na hali ya ushindani ya kutosha,” alisema Mgunda na kuongeza;

“Tunahitaji kwenda Angola tukiwa katika hali nzuri na morali ya kupata ushindi ili kuhakikisha huko ugenini tunapata matokeo bora katika mchezo huo kabla ya kuja kukamilisha kazi hiyo hapa nyumbani ili kutinga hatua ya makundi kama malengo yetu yalivyo,”alisema Mgunda ambaye hivikaribuni alisainishwa mkataba wa mwaka mmoja na atakuwa msaidizi wa Kocha mpya wa Simba ambaye mchakato unakwenda kimyakimya. Mgunda ametokea kukubalika na mashabiki wa Simba kutokana na matokeo yake.