Prime
Kinachoisubiri Simba kwa Waarabu hiki hapa

Muktasari:
- Kwenye michezo minne ambayo Simba ilipoteza ugenini mmoja ilicheza Algeria ikipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya ES Sétif, Aprili 6, 2012.
Simba imeenda Algeria huku ikiwa na kumbukumbu mbaya za kupata matokeo kwenye michezo ya ugenini hususani pale inapokutana na timu za Waarabu ambapo mara ya mwisho Simba kwenda Algeria ilikuwa Machi 9, 2019 ilipopoteza mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura.
Kwenye Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba imecheza michezo sita ikiwa ugenini dhidi ya timu za Waarabu ambapo imepata sare michezo miwili huku ikipoteza michezo minne.
Kwenye michezo minne ambayo Simba ilipoteza ugenini mmoja ilicheza Algeria ikipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya ES Sétif, Aprili 6, 2012.
Michezo mingine ambayo Simba ilipoteza ugenini ilikuwa Mei 8, 2010 ilipofungwa mabao 5-1 dhidi ya Haras El-Hedood ya Misri, Mei 13, 2012 ilipoteza ugenini mabao 3-0 dhidi ya Al-Ahly Shendi ya Sudan huku mara ya mwisho kwenye Kombe la Shirikisho Simba ilipoteza Uarabuni Februari 27, 2022 ilipofungwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Katika michezo minne ambayo Simba ilipoteza ugenini vilevile ilifanikiwa kupata ushindi ilipokuwa nyumbani ambapo mara ya mwisho ilicheza na Al Ahli Tripol ya Libya ikiifunga mabao 3-1, Septemba 22, 2024 huku mechi ya mwisho kwenye makundi ilicheza dhidi ya RS Berkane ikishinda bao 1-0 Machi 13, 2022.
Simba ilipata sare dhidi ya Al-Masry kwenye michezo yote miwili iliocheza nyumbani na ugenini ambapo Machi 7, 2018 ilipata sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kwenda Misri Machi 17, 2018 ilipolazimishwa sare ya 0-0 kama ilivyofanya dhidi ya Al Ahli Tripoli Septemba 15, 2024.
Kikosi cha Simba kimeanza safari alfajiri ya leo Jumatano Desemba 5, 2024 kwenda Algeria ambapo itacheza mchezo wa pili hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine.
Simba imeondoka na nyota 22 kwenda kuzisaka pointi tatu nyingine kwenye mchezo utakao chezwa Uwanja wa Mohamed Halaoui Desemba 8, mwaka huu kuanzia saa 1:00 usiku.
Huu utakuwa mchezo wa pili kwa timu zote mbili ikiwa Simba ilicheza mchezo wa kwanza dhidi ya FC Bravos na kushinda kwa bao 1-0 huku CS Constantine ikishinda dhidi ya CS Sfaxien kwa bao 1-0 ugenini.
Simba imepangwa kundi A ikiwa na pointi tatu nafasi ya pili, CS Constantine inaongoza kundi ikiwa na pointi tatu wakati Bravos na CS Sfaxien zikishika nafasi ya tatu na nne.
Kikosi cha Simba Kilichoenda Algeria
Magolikipa
Aishi Manula, Moussa Camara, Ally Salim
Mabeki
Che Fondoh Malone, Karaboue Chamou, Abdurazak Hamza,Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Valentin Nouma, Kelvin Kijili
Viungo
Mzamiru Yassin, Debora Fernandez, Fabrice Ngoma, Ladaki Chasambi, Augustine Okejepha, Omary Omary,Edwin Balua, Kibu Denis,Jean Charles Ahoua, Awesu Awesu
Washambuliaji
Steven Mukwala, Leonel Ateba
Msimamo wa kundi A
1. CS Constantine - 3
2. Simba - 3
3. FC Bravos - 0
4. CS Sfaxien - 0