Kipa Coastal: Mayele alinilaghai

Muktasari:

  • KIPA wa Coastal Union, Mussa Mbisa amesema bao la kichwa alilofunga Fiston Mayele, alimlaghai kwani alidhani angepiga upande ambao aliruka lakini alijikuta anapishana na mpira.

KIPA wa Coastal Union, Mussa Mbisa amesema bao la kichwa alilofunga Fiston Mayele, alimlaghai kwani alidhani angepiga upande ambao aliruka lakini alijikuta anapishana na mpira.

Alisema wakati anawahi kuudaka, Mayele alielekeza kichwa upande mwingine na kupiga mpira juu zaidi, hivyo alijikuta anaruhusu nyavu zake kutikiswa.

“Nikizungumzia mechi na Yanga kwa jumla ilivyokuwa, bao la Mayele ndilo liliwapa nguvu, ila kiukweli mpira usingekuwa na mabao, Coastal Union tumecheza vizuri zaidi,” alisema na aliongeza;

“Wakati anapiga kichwa akipokea asisti ya Djuma Shaban alinitazama kama anaupiga katikati, akapiga kichwa kwenda pembeni na nilifanya jitihada za kuokoa, lakini ndio soka, najipanga kwa mechi zijazo,”alisema.

Alisema ligi bado ni ndefu na kama kipa anapaswa kuwasoma washambuliaji kila wakati ili kuhakikisha anakuwa msaada kwa timu yake kutoshambuliwa sana. “Ujue kuna washambuliaji kutoka timu nyingine nje ya Simba, Yanga na Azam FC wanafunga mabao mazuri sana, ila kwa sababu hawana mashabiki ndio maana huwezi kuwagundua mapema, nimemtaja Mayele kwa sababu nazungumzia mechi hiyo,” alisema.

Mayele aliwahi kuzungumzia jina lake hilo (Mayele), lina maana mtu mwenye akili na ndio maana anafunga mabao kwa kutumia akili kubwa.