Klabu Ligi Kuu "zaichokonoa" TFF
Muktasari:
Awali, klabu zilitoa tamko la kutocheza ligi mzunguko wa pili zikidai kwanza kulipwa kwa fedha za udhamini zilizoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki huu, huku klabu zikitoa masharti magumu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ligi hiyo inayozishirikisha timu 14, imepangwa kuendelea na mzunguko wa pili Januari 26, baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza Novemba mwaka jana.
Awali, klabu zilitoa tamko la kutocheza ligi mzunguko wa pili zikidai kwanza kulipwa kwa fedha za udhamini zilizoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Jana Ofisa habari wa TFF, Bonifance Wambura alisema kuwa katika kikao cha pamoja walichoketi TFF na Kamati ya Ligi waliafikiana kucheza ligi kwa masharti.
Wambura alisema masharti hayo yalikuwa yawasilishwe kwa barua kutoka kamati hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallance Karia alisema tayari wameshawasilisha masharti yao kama ilivyopendekezwa kwenye kikao.
Kwa mujibu wa Karia, moja ya sharti lao ni kuzuia mgao wa udhamini kutoka Kampuni ya Huduma za Simu za Mikononi (Vodacom) kwenda TFF.
Udhamini huo ni kiasi cha Sh80 milioni kwa vipindi viwili tofauti Ligi.
Akifafanua, Karia alisema TFF inadaiwa na klabu za Ligi Kuu kiasi cha Sh117 milioni kama mgawo wa udhamini wao baada ya TRA kukata Sh157 milioni kutoka fedha za udhamini.
�Katika hizo, zilizosalia kila klabu inapata kiasi Sh10 milioni za udhamini,� alisema Mwenyekiti Karia wakati akiongea na Mwananchi.
Mbali na kutaka kuzuia mgawo huo, pia wanataka kupewa asilimia tano ya mapato ya mlangoni wanayochukua TFF kila mechi.
Aidha, sharti lingine ni kutaka asilimia 10 ya mapato ya uwanja yanayokwenda serikalini wapewe mpaka deni litakapomalizika.
Mzunguko huo wa pili unaanza kwa bingwa mtetezi, Simba kucheza na African Lyon, huku Yanga wanaoongoza ligi wakishuka dimbani Januari 27, kucheza na Prisons. Mechi nyingine siku hiyo zitakuwa, Mtibwa Sugar dhidi ya Polisi Moro kwenye Uwanja wa Manungu, huku Coast Union wakicheza na Mgambo Uwanja wa Mkwawani.
Ruvu Shooting watakwaruzana na JKT Ruvu Uwanja wa Mabatini, Azam wakiwakaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Chamanzi na JKT Oljoro dhidi ya Toto African, Sheikh Amri Abeid.