Klopp apokewa kifalme Anfield

Kikosi cha Liverpool pamoja na kushindwa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kimepokelewa kifalme kwenye Uwanja wa Anfield ukiwa ni mchezo wa mwisho wa kocha Jurgen Klopp wakati wakivaana na Wolves.

Kundi kubwa la mashabiki limeonekana likiwa barabarani na bendera pamoja na picha mbalimbali zikimuonyesha kocha huyo aliyefanya mambo makubwa katika kikosi hicho tangu alipojiunga nacho.

Huu ni mchezo wa mwisho wa Klopp kwenye kikosi hicho baada ya kutangaza awali kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu huu.

Kundi hilo la mashabiki lilikuwa likiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu kocha huyo pamoja na wachezaji wa Liverpool ambao wapo kikosini kwa sasa.

Liverpool tayari wana uhakika wa kumaliza kwenye tatu bora ikiwa imekusanya pointi 79 kwenye michezo 37 ya Ligi Kuu England waliocheza hadi sasa.

Kwenye miaka tisa ambayo kocha huyo amekaa Liverpool, ameweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA, na Kombe la Ligi. Pia kocha huyo ameshatwaa Klabu Bingwa Dunia pamoja na Uefa Super Cup.

Klopp ambaye alichukua nafasi ya Brendan Rodgers mchezo wa leo ni wa 489.