Kocha Bilo afariki uwanjani Mwanza, wadau wamlilia
Aliyewahi kuwa Kocha wa timu kadhaa nchini, Athuman Bilali 'Billo' amefariki dunia. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Bilo katika uhai wake amefundisha timu kadhaa ikiwamo Toto Africans aliyoichezea pia, Gwambina FC, Alliance FC na hadi anakutwa na umauti alikuwa mmliki wa kituo cha michezo cha Bilo Sports chenye timu ya Bilo Queens ya Ligi Kuu ya Wanawake.
Aliyewahi kuwa Kocha wa timu kadhaa nchini ikiwamo Stand United 'Chama la Wana', Pamba (kwa sasa Pamba Jiji), Athuman Bilali 'Billo' amefariki dunia huku chanzo kikiwa hakijafahamika.
Billo hadi anakutwa na umauti alikuwa anamiliki kituo cha michezo na timu ya Bilo Queens ya Ligi Kuu ya Wanawake.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo amethibitisha kufariki kwa kocha huyo akieleza kuwa ni masikitiko makubwa kwa wadau na mashabiki wa soka mkoani humo na Tanzania kwa ujumla.
Amesema taarifa za awali zinadai kuwa kocha huyo jana Aprili 15 aliendelea na shughuli zake za mazoezi na timu yake Bilo Queens katika uwanja wa Shule ya Msingi Nyasaka jijini humo hadi jioni licha ya kwamba wachezaji walimuacha eneo hilo amekaa.
"Jana alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na timu yake ila hadi wanaondoka wachezaji wakamuacha amekaa hadi kukutwa asubuhi amefariki hapohapo.
"Bado hatujajua chanzo zaidi kwa kuwa yupo hospital tutafahamu kwa ujumla ikiwamo ratiba na taratibu nyingine za mazishi, lakini kwetu wadau na mashabiki ni pigo," amesema Malongo.