Kocha Maximo amtwisha Nsajigwa zigo la Kagame
Kocha mpya wa timu ya vijana ya Yanga, Shadrack Nsajigwa (katikati) akiwaelekeza wachezaji wake pamoja na wachezaji wa timu ya wakubwa, walipokuwa wakifanya mazoezi ya pamoja kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Maximo anaona kuwa bado kikosi chake hakijawa fiti kwa ajili ya michuano hiyo.
Dar es Salaam. Katika hali inayoonekana kuwa na hofu ya kuchafua rekodi yake mapema Kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo ameikacha michuano ya Kagame kwa kumpa jukumu kocha wa timu ya vijana, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ kuhakikisha anarudi na ubingwa wa Kombe la Kagame.
Maximo ambaye ameinoa Yanga tangu mwezi uliopita aliliambia gazeti hili kuwa ameshagawa timu mbili kwa malengo tofauti, moja iliyo na vijana wengi na baadhi wazoefu itakwenda Kagame na nyingine atabaki nayo yeye kambini Pemba kujiandaa na ligi.
“Nimeshateua timu itakayokwenda Rwanda na itakuwa chini ya kocha Nsajigwa na Leonardo Neiva wakati nyingine nitabaki nayo mimi na Salvatory ambayo tutakwenda Pemba, lengo ni kuhakikisha naiandaa timu kikamilifu kwa ajili ya Ligi Kuu.”
Maximo ameamua kuipeleka timu ya vijana kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika Mashariki na Kati itakayoanza Agosti 8, huku akiongeza wachezaji sita kutoka timu ya wakubwa.
“Nitaongeza mchezaji mmoja au wawili kati ya wale walioko Taifa Stars ambaye naye atakwenda kwenye michuano ya Kagame kuongeza nguvu ingawa siwezi kumtaja ni mchezaji gani kwa sasa,” alisema Maximo.
Katika mazoezi ya wiki hii Maximo alionekana kuiandaa kikamilifu timu itakayoshiriki michuano ya Kagame huku akiamini kuwa itafanya vizuri na kurudi na ubingwa.
Kwa mujibu wa mazoezi hayo wachezaji wa timu kubwa watakaoongozana na timu ya vijana ni Nizar Khalfan, Omega Seme, Hussein Javu, Rajab Zahir, Said Bahanuzi na kipa Ali Mustapha ‘Barthez.’
Yanga imepangwa kundi moja na Rayon Sports ya Rwanda, Atlabara na KMKM ya Zanzibar.