Kumng’oa Mayele Sh8 bilioni, Pyramids wakomaa naye
Muktasari:
- Mayele aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambao alipachika mabao sita.
Dar es Salaam. Pyramids ya Misri imeweka bei ya Doła 3 milioni (Sh8 bilioni) kwa timu inayomhitaji mshambuliaji Fiston Mayele katika kipindi cha dirisha hili la usajili.
Mayele aliyeongoza kwa kufumania nyavu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akipachika mabao sita, anawindwa na klabu kadhaa za ndani na nje ya Afrika.
Katika kundi hilo la timu zinazomhitaji Mayele, Al Fateh ya Saudi Arabia ndio inayotajwa kuwa mstari wa mbele kwa vile tayari imeshawasilisha ombi kwa Pyramids FC kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji huyo.
Timu nyingine inayoripotiwa kumnyemelea kwa udi na uvumba Mayele ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Vyombo mbalimbali vya habari nchini Misri, vimeripoti kwamba Pyramids itakuwa tayari kumuachia Mayele ikiwa itapokea kiasi kisichopungua Doła 3 milioni vinginevyo nyota huyo wa zamani wa Yanga na AS Vita Club atabakia klabuni hapo.
Hata hivyo inaripotiwa kwamba Al Fateh inaweza kurudi nyuma katika harakati za kumsaka Mayele kwa vile inaona kiasi hicho cha fedha kinachohitajika na Pyramids FC hakiendani na thamani halisi ya mshambuliaji huyo.
Al Fateh inaamini kwamba Mayele anatakiwa kuuzwa kwa gharama ya chini ya fedha hizo ambazo Pyramids FC inazihitaji.
Mkataba wa Mayele na Pyramids FC utafikia tamati mwishoni mwa msimu ujao na inaripotiwa kwamba nyota huyo kutoka DR Congo ameshaonyesha nia ya kutafuta changamoto mpya kwingine.
Mabao ya Mayele katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita yalitoa mchango mkubwa kuiwezesha Pyramids FC kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ikiwa ni mara ya kwanza kwao kufanya hivyo.
Mayele pia aliisaidia Pyramids FC kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Misri katika msimu uliopita ambapo alifumania nyavu mara sita katika mechi 17.
Kiujumla tangu Mayele alipojiunga na Pyramids FC mwaka 2023, ameifungia mabao 57 katika michezo 112 huku akipiga pasi 13 za mabao.