Kutana na masela waliotaka kumtenga Samatta

Sunday May 02 2021
pazia pic 2
By Edo Kumwembe

KUNA masela matajiri walikutana mahala. Sijui ni Paris au Madrid, ama London au wapi. Inawezekana walikutana fukwe za Miami wakiwa na zile sigara kubwa za Wazungu maarufu kama Cigar. Kando walikuwa na mivinyo yao huku wakitabasamu.

Walipanga kuuficha mpira wetu. Wahuni sana. Nawazungumzia matajiri wa Real Madrid, Arsenal, Manchester United, Real Madrid, Chelsea, Manchester City, Juventus, AC Milan, Inter Milan, Liverpool, Barcelona. Wahuni sana hawa watu. Walikuwa wakiongozwa na Florentino Perez.

Walitaka kuanzisha ligi yao. Ligi ya matajiri. Kwamba kila katikati ya wiki wangekuwa wanacheza wenyewe kwa wenyewe. Hapohapo walitaka ligi zetu pendwa ziendelee, lakini katikati ya wiki wangekuwa wanacheza wenyewe kwa wenyewe katika michuano ambayo haushuki daraja.

Hii ilikuwa na maana kusingekuwepo na michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na ile ya Europa. Wao ndio wangekuwa wameupora usiku wa Ulaya na kutuletea michuano ya kufikirika. Wazungu wanaita ‘Fantasy football’.

Wangetengeneza pesa nyingi katika michuano hii, lakini wangepunguza msisimko wa soka. Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni michuano ya kiasili. Ina historia yake. Jaribu kufikiria. Arsenal haijawahi kutwaa ubingwa wa Ulaya na wanapambana kuchukua taji hili walau kwa mara ya kwanza. Vipi wangeenda katika michuano hiyo na kuchukua. Unadhani wangepata msisimko kama ambao wataupata wakichukua michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika muundo wa sasa?

Masela wetu wangepata pesa, lakini vipi ligi nyingine nyingi za Ulaya. Unadhani Ligi Kuu ya Croatia ingekuwa na msisimko tena wakati bingwa wake atakuwa anakwenda katika michuano ya Ulaya ambayo haina Real Madrid, Barcelona, Manchester United na wengineo?

Advertisement

Ina maana kina Leicester City ndio wangekuwa wababe wa michuano ya Ulaya au sio? Ina maana kina Madrid wangekuwa hagusi tena Stockholm kwenda kucheza na timu za kule ambazo zimefuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Udhamini wa michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ungepungua kwa sababu wakubwa hawapo. Mashabiki wangepungua katika viwanja mbalimbali kwa sababu timu za masela haziendi tena katika viwanja vyao. Kila katikati ya wiki wangekuwa wanacheza wao kwa wao.

Ni kweli wangekuwa wanapata pesa nyingi, lakini unadhani West Ham wangekuwa wanapambana kwa nguvu zote kwa ajili ya kuingia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambayo ingewawezesha kucheza na Napoli tu?

Hapana. Ni ndoto za mashabiki wa West Ham kusafiri mpaka Nou Camp kuiona timu yao ikicheza Barcelona. Na ndio maana sasa hivi wanapambana kufa na kupona kuingia katika Top Four. Huu ndio msisimko wa mchezo wa soka.

Wazo kama hili la masela Wazungu wasio wabinafsi walikuwa nalo miaka ya 1940, ndio maana wakaanzisha Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo walijumuisha timu mbalimbali na sio timu za masela peke yao. Leo masela wamekuwa wakubwa zaidi na wanataka kuwatenga wenzao. Sio sawa.

Wazo hili pia lingemfanya Mbwana Samatta asicheze katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Asingegusa Anfield. Timu yake ya zamani Genk isingekuwepo katika michuano ya matajiri kwa sababu hakuna timu yoyote ya Ubelgiji ambayo ilijumuishwa na matajiri.

pazia pic

Hata timu yake ya sasa isingegusa Old Trafford, Anfield, Emirates, Santiago Bernabeu na kwingineko kwa sababu Fenerbahce haipo katika orodha ya timu za masela. Hawa ndicho walikuwa wanataka kuufanya mpira wetu.

Wazungu walioanzisha Ligi ya Mabingwa Ulaya hawakuwa wachoyo, lakini Wazungu hawa waliokutana majuzi walikuwa wahuni na wachoyo. Ndoto za vijana wengi kuanzia London, Tanga, Capetown, Buenos Aires kucheza katika viwanja vikubwa duniani wakiwa na timu za kawaida zingepotea.

Hata mashabiki wa timu za masela waliona wazi kwamba huu ulikuwa uonevu dhidi ya timu za kawaida. Na kwa jinsi wasivyo wabinafsi wakaamua kuandamana kuwasaidia wenzao ili waweze kukutana katika viwanja mbalimbali duniani.

Kitu pekee ambacho naamini masela wanaweza kujitetea kwa sasa ni kwamba labda walitumia mbinu hii kwa ajili ya kupata maslahi zaidi kutoka Uefa. Labda lilikuwa shinikizo la chinichini kwa ajili ya kuhakikisha Uefa inawalipa zaidi.

Sina tatizo kama Uefa itawalipa zaidi kuliko wadogo wengine, lakini kujitoa kabisa katika michuano hii ni jambo ambalo halikubaliki. Ndoto ya mashabiki wa Wolves ni kuwaona kina Sergio Ramos, Lionel Messi, Neymar na wengineo wakicheza katika dimba la Molineux.

Masela wamefanya jambo baya sana. Haikuwa sawa na bahati nzuri ni kwamba na wenyewe wamejua kwamba haikuwa sawa na ndio maana wamekwenda mbali zaidi kwa kuomba radhi, licha ya kujitoa katika mpango mzima. Wamefanya jambo la maana ingawa kwa sasa inabidi tuanze kuwaangalia kwa jicho la pembeni.

Kitu ambacho sina uhakika nacho ni kama mechi zao zenyewe zisingetukifu. Huenda tungezichoka. Katika fikra unaweza kudhani kwamba mechi zao zingesisimua sana, lakini sijawahi kuamini kwamba ukila pilau kila siku ni jambo jema.

Kwa mfano, mechi nyingi zisingekuwa zinatoa maajabu. Leo Madrid kumfunga Barcelona sio maajabu, lakini kama Dinamo Zagreb inamfunga Real Madrid pale Santiago Bernabeu basi yanakuwa maajabu na mchezo wa soka unaendelea kuwa mchezo unaosisimua zaidi.

Masela walikuwa wanataka kufanya jambo baya katika soka. Walikuwa wanataka kutuletea fainali ya Leicester City dhidi ya Benfica katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Walikuwa wanataka Mwanasoka Bora wa Dunia awe James Madisson kitu ambacho sio haki katika dunia ambayo ina Kelvin Mbappe, Lionel Messi, Neymar na wengineo. Masela sio watu.

Advertisement