Ligi Kuu Bara maji na mafuta yanajitenga
Muktasari:
- Kagera Sugar ndiyo inayoburuza mkia baada ya kuanza vibaya msimu huu ambapo imecheza mechi tatu na kupoteza zote.
Dar es Salaam. Tangu pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kufunguliwa Agosti 16, 2024 timu mbalimbali ziliendelea kuonyeshana ubabe katika kutafuta pointi tatu kwenye mechi zake.
Kagera Sugar ndiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo baada ya kuanza vibaya msimu huu ambapo imecheza mechi tatu na kupoteza zote.
Mechi ya kwanza Kagera ilicheza Agosti 24, 2024, ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Kaitaba Mkoani Kagera baada ya kuruhusu bao la dakika za jioni lililofungwa na Anthony Tra Bi Tra raia wa Ivory Coast.
Mechi ya pili ilichezwa siku tano baadaye, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, ambapo iliruhusu kipigo cha mabao 2-0 yaliyofungwa na Max Nzengeli dakika ya 25 pamoja Clement Mzize akifunga dakika ya 89.
Mechi ya tatu, ilichezwa Septemba 9, 2024, ilipokuwa ugenini dhidi ya Tabora United alikuwa ni Shedrack Ausiegbu kiungo mpya kutoka Rivers United ya Nigeria ndiye aliyezamisha mpira wavuni Kagera Sugar wakifungwa bao 1-0.
Timu nyingine ambayo haijapata ushindi ni Namungo ambayo ilicheza mechi zote mbili kwenye Uwanja wa nyumbani wa Majaliwa ambapo mchezo wa kwanza ilicheza na Tabora United ikipoteza kwa mabao 2-1, huku mchezo wa pili ikicheza na Fountain Gate ikipoteza kwa mabao 2-0 na mchezo wa tatu ulipigwa jana Septemba 12, 2024 dhidi ya Dodoma Jiji ambapo ilipoteza kwa bao 1-0
KenGold iliyopanda daraja msimu huu ikitokea Championship nayo ina hali mbaya, ikiwa imepoteza michezo miwili baina ya Singida Black Stars Agosti 18, ikipoteza kwa mabao 3-1 na mechi nyingine ilipoteza dhidi ya Fountain Gate Septemba 11, ikifungwa mabao 2-1, Septemba 16, 2024 itavaana na KMC, iwapo ikipoteza itaungana na Kagera Sugar pamoja na Namungo zilizopoteza michezo mitatu ya mwanzo.
Matokeo waliyopata Kagera Sugar kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu, yanaifanya timu hiyo kuwa nafasi ya mwisho kwenye msimamo ikiwa imefungwa mabao manne huku yenyewe ikiwa haijafunga bao hata moja tofauti na Namungo ambayo imeruhusu mabao matano huku ikifunga bao moja tangu msimu uanze.
Hii ni ishara mbaya kwamba kwenye michezo 27 iliyobaki ya Ligi Kuu timu hizo zinatakiwa kuhakikisha kuwa zinapata ushindi kwenye mechi zao ili kujiokoa na janga la kushuka daraja.
Timu ya Singida Black Stars yenyewe inaongoza Ligi Kuu ikiwa imeshinda mechi zake zote tatu, ikiwa ndiyo timu pekee ambayo imecheza michezo mitatu na kushinda yote, ikifuatiwa na Simba ambayo inashika nafasi ya pili baada ya kucheza michezo miwili na kushinda yote ikiwa na pointi sita, timu ya tatu ni Singida Fountain ambayo imecheza michezo mitatu na kushinda miwili sawa na Tabora United iliyopo nafasi ya nne.
Timu mbili pekee ndiyo zimetoka sare michezo yote miwili ambayo zimecheza, Pamba ina pointi mbili baada ya sare ya michezo miwili sawa na Prisons, huku Coastal, Azam, JKT Tanzania na KMC zikiwa zimecheza mchezo mmoja mmoja na zimetoka sare, hivyo kila moja ina pointi moja.
Yanga pekee ndiyo imecheza mchezo mmoja na kushinda hivyo kukusanya pointi tatu ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Hadi sasa Simba ndiyo inaongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi ikiwa imefunga saba moja mbele ya Singida ambayo imefunga sita kwenye michezo mitatu, Fountain inafuata ikiwa imefunga mabao manne, Tabora matatu, Yanga KMC na KenGold zimefunga mawilimawili.
Kwenye michezo hiyo, Pamba, Prisons, Azam, JKT Tanzania pamoja na hazijafunga bao lolote hadi sasa, huku Singida, KenGold na Namungo zikiwa zinaongoza kwa kufungwa mabao mengi baada ya kuruhusu matano kila moja.