Liverpool yakabidhiwa kombe la 20, Alexander-Arnold aagwa
Muktasari:
- Majogoo hao wa Anfield wamefunga msimu kwa kukusanya jumla ya pointi 84 juu ya Arsenal yenye pointi 74, Man City (71), Chelsea (69) na Newcastle United (66).
Klabu ya Liverpool imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) na kuifanya kufikisha makombe 20 ya ligi sawa na Manchester United.
Liverpool ambayo imefunga msimu wa 2024/25, kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Crystal Palace ilitangaza ubingwa zikiwa zimesalia mechi nne kufikia tamati ya ligi hiyo.
Katika mechi ya leo Jumapili Mei 25, 2025, Liverpool imelazimisha sare baada ya kutanguliwa na Palace kufuatia bao lililofungwa na Ismaila Sarr (9’) kabla ya Mohamed Salah kuisawazishia Liverpool dakika ya 84.
Hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
Baada ya dakika 90, Liverpool imekabidhiwa kombe katika hafla iliyoshuhudiwa na mashabiki zaidi ya 60,000 wakiongozwa na wakongwe wa timu hiyo wakiongozwe Steven Gerrard.
Pia kocha wao mstaafu, Jurgen Klopp alisafiri kutoka Salzburg nchini Austria kushuhudia vijana wake wa zamani wakinyanyua makwapa.
Salah na tuzo
Huku shangwe likiwa kila mahali ndani na nje ya Uwanja wa Anfield kwa majogoo hao, mchezaji wao Mohamed Salah ameibuka kinara wa ufungaji wa mabao kwa kufunga mabao 29 mbele ya straika wa Newcastle United, Alexander Isak (23) na Erling Halaand mwenye mabao 22.
Kutokana na kuongoza katika orodha ya ufungaji wa mabao ametwaa kiatu cha dhahabu. Pia ametwaa tuzo ya mchezaji mwenye 'asisti' nyingi akifikisha 18.
Kutokana na tuzo hizo, Mohamed Salah amevunja rekodi ya kuhusika kwenye mabao mengi akimfikia Alan Shearer aliyefanya hivyo msimu wa 1994/95.
Mbali na Salah, mchezaji wa Liverpool, Ryan Gravenbech ametwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa ligi hiyo.
Katika sherehe hizo, beki wa kulia, Trent Alexander-Arnold ameaga rasmi na kupewa baraka na mashabiki wa Liverpool. Trent anaenda kujiunga na miamba wa Hispania, Real Madrid.