Mabao ya kujifunga yashamiri Brazil

Beki wa Marekani, Fabian Johnson (kushoto) akijaribu kumzuia beki wa Ghana, Jonathan Mensah (kulia) asipige mpira wakati wa mchezo wa Kundi G uliofanyika kwenye Uwanja wa Dunas, Natal. Ghana walifungwa 2-1. Picha na AFP
Muktasari:
Jumla ya mabao ya kujifunga yamefikia nusu ya rekodi ya magoli sita yaliyofungwa 1998.
Salvador, Brazil. Dunia imeshuhudia mabao mengi ya kujifunga katika siku nne za kwanza za fainali za Kombe la Dunia 2014 kuliko yaliyofungwa katika fainali za 2010.
Jumla ya mabao ya kujifunga yamefikia nusu ya rekodi ya magoli sita yaliyofungwa 1998.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia katika mchezo wa ufunguzi kuwepo na bao la kujifunga kwa wenyeji baada ya Marcelo kujifunga na kuifanya Brazil kuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Croatia. Hata hivyo Brazil walifanikiwa kusawazisha na baadaye kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Tangu Manuel Rosas wa Mexico alipojifunga katika mechi ya Kombe la Dunia 1930, ni wachezaji 39 wamejifunga pamoja na makipa.
Bulgaria imejifunga mara mbili katika Kombe la Dunia 1966 na kulazimisha sare dhidi ya Hispania na Mexico kwa kujifunga. Ujerumani na Italia wamefaidika kwa mabao hayo mara nne.
Bao la kujifunga lililojizolea umarufu ni lile la 1994 wakati Colombia, iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kunyakuwa ubingwa, ilipojikuta ikijilaumu baada ya nahodha wao, Andres Escobar kujifunga.
Bao hilo liliifanya Marekani kuongoza kwa 1-0 kabla ya kushinda 2-1. Bao la kujifunga Escobar liligharimu maisha ya mchezaji huyo baada ya kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa walipoteza fedha zao katika kamari kutokana na Colombia kupoteza mchezo huo.
Mabao mawili ya kujifunga mwaka huu yalitokea Jumapili, wakati beki wa Bosnia, Sead Kolasinac alipojifunga dhidi ya Argentina kabla ya kipa wa Noel Valladares wa Honduras kujifunga dhidi ya Ufaransa.
Bao la kujifunga Kolasinac liliigharimu zaidi Bosnia walionyukwa mabao 2-1 na Argentina. Goli hilo ni la 14 kwa timu kujifunga na kupoteza mchezo wa Kombe la Dunia. Kwa kawaida matokeo huwa ni sare au ushindi kwa timu iliyojifunga.
Hii ni mara ya nne katika historia ya Kombe la Dunia kufungwa mabao mawili ya kujifunga siku ya Jumapili. Tukio kama hilo lilitokea Juni 21, 1978 na Juni 10, 1998. Mwaka 2002, Marekani na Ureno walipoteza nafasi ya kusonga mbele baada ya kujifunga.
Beki wa Uholanzi, Ernie Brandts ni mchezaji pekee aliyejifunga na kufanikiwa kufuta kosa lake kwa kufunga bao la kusawazisha. Alijifunga katika mechi dhidi ya Italia ilipoongoza 1-0 mwaka 1978.
na kusawazisha kosa lake kwa kufunga bao moja wakati Uholanzi iliposhinda 2-1.