Mabondia Juma Choki, Tony wawekewa gari mezani
Dar es Salaam. Pambano kuu la Dar Boxing Derby 2026 kati ya Juma Ramadhan Choki na Tony Rashid limepata msisimko mpya baada ya waandaaji kutangaza kuwa mshindi atajinyakulia gari aina ya Toyota Crown New Model, hatua iliyolenga kuongeza thamani ya mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Waandaaji wa pambano hilo, Pick Time Media kwa kushirikiana na Major Semunyu, wamesema zawadi hiyo imewezekana kupitia wadhamini Euromax Limited, Distinction Limited, QFK Motor, Azam TV na PK Pharmacy huku wakieleza kuwa gari hilo ni bonasi kwa mabondia ambao tayari wamelipwa fedha zao za mapambano kwa mujibu wa mikataba yao.
Pambano hilo litafanyika Julai 24 katika viwanja vya Ubungo East African Logistic Center, Dar es Salaam na linatarajiwa kuvuta mashabiki wengi kutokana na ubora wa mabondia hao pamoja na zawadi hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa zawadi hiyo, Juma Choki alisema amekuwa akiomba Mungu amlinde hadi siku ya pambano ili aweze kuingia ulingoni akiwa katika hali nzuri na kupigania ushindi.
"Ninachomuomba Mungu ni anilinde nisipate majeraha mazoezini wala njiani hadi nifike siku ya pambano. Nina imani nitafanya vizuri na nitaweza kushinda," alisema Choki.
Choki amesema gari hilo linaweza kubadili maisha yake kwa kuwa kwa sasa hutegemea pikipiki kama usafiri wake wa kila siku, akiamini ushindi huo utakuwa chachu kwa mabondia wengine kuona kuwa ngumi zinaweza kuwainua kiuchumi.
"Leo natumia bodaboda kwenda mazoezini. Nikipata gari maisha yangu yatakuwa mepesi zaidi na naamini vijana wengi wataona kuwa kupitia ngumi inawezekana kubadilisha maisha," alisema.
Kwa upande wake, Tony Rashid alisema zawadi hiyo pia ina thamani kubwa kwake kwa sababu hana gari, lakini akasisitiza kuwa haijamuongezea presha yoyote kwani maandalizi yake yamekuwa yakilenga ushindi tangu aliposaini pambano hilo.
"Hakuna bondia anayejiandaa kwenda kushindwa. Gari ni motisha, lakini hata kama lisingekuwepo ningefanya maandalizi haya haya kwa ajili ya kushinda pambano," alisema Rashid.
Mwakilishi wa Distinction Limited ni Danstan Myava alisema kampuni hiyo imeamua kwenda mbali zaidi ya kudhamini gari kwa kuanzisha mpango wa kumfundisha bingwa wa pambano biashara kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita ili aweze kuwa na chanzo kingine cha kipato wakati na baada ya maisha ya ngumi.
"Tunataka zawadi hii isiishie kuwa gari pekee. Tutamfundisha bingwa namna ya kufanya biashara ili ajenge maisha yake hata baada ya kuachana na ndondi," amesema mwakilishi huyo.
Naye mwakilishi wa Euromax Limited ambao ni wazalishaji wa Smart Gin, Peter Michael amesema kampuni hiyo imekuwa ikiunga mkono maendeleo ya ngumi tangu mwaka 2017 na safari hii imeamua kushirikiana na Distinction Limited kuwajengea mabondia uwezo wa kujiajiri.
"Hii si zawadi ya gari tu. Tunataka kufungua ukurasa mpya ambapo mabondia watakuwa na biashara na vyanzo vya uhakika vya mapato hata baada ya kustaafu mchezo wa ngumi," amesema Peter.
Kwa upande wa PK Pharmacy, Dk Omari Semunyo amesema wamejipanga kuhakikisha usalama wa mabondia ndani na nje ya ulingo, akisisitiza kuwa afya ya bondia ndiyo kipaumbele kwa kuwa "kuna maisha baada ya ngumi."