Madega afariki dunia
Muktasari:
- Madega amefariki dunia baada ya kusumbuliwa na tatizo la presha kwa muda mrefu ambapo kesho atazikwa nyumbani kwakwe Chalinze.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega amefariki dunia leo wakati akipatiwa matibabu katika Hospital ya Wilaya ya Chalinze, Musoga.
Kifo cha Mwenyekiti huyo kimethibitishwa leo Jumamosi Februari 10, 2024 na mwanaye, Abdul Madega alipozungumza na Mwananchi kwa simu.
Amesema baba yake alimpigia simu asubuhi na kumweleza kuwa anajisikia vibaya na kumwambia ampeleke Hospital ya Wilaya ya Chalinze, Musoga.
"Leo asubuhi mzee alinipigia simu kuniambia anajisikia vibaya nimpeleke hospitali, nikafika nyumbani, lakini alikuwa anatembea na nguvu zake kabisa, tukafika hospitali akaanza kutibiwa maradhi ya presha,"
"Akawa anaendelea vizuri tu, baada ya kufika saa tano asubuhi, akaaga dunia,” amesema Abdul.
Kijana huyo amesema kifo cha baba yake kimewashtua watu wengi kwasababu juzi alitoka Dar es Salaam na alipita kwa marafiki zake wengi kuwasalimu akiwa mzima wa Afya, japo amekuwa na tatizo la presha ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Madega anatarajiwa kuzikwa kesho saa 10:00 jioni nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani.