Maguire aweka sharti kusaini mkataba mpya Man United
Muktasari:
- Maguire alijiunga na Manchester United mwaka 2019 akitokea Leicester City kwa ada ya paundi 80 milion (Sh275 bilioni).
Manchester, England. Beki wa Manchester United, Harry Maguire yupo hatua za mwisho kukubaliana na klabu hiyo kuongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja, huku akisisitiza kuwa anataka kuthaminiwa ndani ya kikosi kabla ya kusaini rasmi.
Maguire, mwenye umri wa miaka 33, ambaye mkataba wake wa sasa unaelekea kuisha mwishoni mwa msimu huu, ameendelea na mazungumzo na uongozi wa klabu katika wiki za hivi karibuni. Inaelezwa kuwa makubaliano hayo yatakuwa ya mwaka mmoja na chaguo la kuongeza mwaka mwingine.
Akizungumza akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya England, Maguire ameeleza matumaini yake ya kufikia makubaliano haraka, akisisitiza kuwa uamuzi huo lazima uwe na manufaa kwa pande zote mbili.
“Naamini tutafikia makubaliano ambayo ni mazuri kwa klabu na kwangu pia. Mambo yatawekwa sawa hivi karibuni, iwe nitaendelea kubaki au kuondoka,” amesema beki huyo.
Licha ya kuondolewa unahodha wake, Maguire ameweka wazi kuwa bado ana mapenzi makubwa na klabu hiyo ya Old Trafford, lakini hataki kubaki kwa sababu za kihisia tu.
“Naipenda klabu hii, lakini lazima iwe sahihi kwangu na kwa klabu pia. Sitaki kubaki kwa sababu ya hisia. Nataka kubaki kwa sababu klabu inanihitaji na inaamini nina mchango mkubwa,” ameongeza.
Maguire pia amerejea katika kikosi cha England chini ya kocha Thomas Tuchel, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uteuzi wa kikosi cha mwisho cha Kombe la Dunia.
Kocha wa Manchester United, Michael Carrick amemsifu Maguire akimtaja kama mchezaji mwenye moyo wa kupambana na kiongozi ndani ya kikosi, licha ya changamoto alizowahi kupitia.
Maguire alijiunga na Manchester United mwaka 2019 akitokea Leicester City kwa ada ya paundi 80 milion (Sh275 bilioni), na tangu wakati huo amekuwa mmoja wa mabeki wenye uwezo mkubwa ndani ya kikosi hicho.