Wakala wa Sesko akataa jina la ‘super sub’
mshambuliaji wa Manchester United, Benjamin Sesko akiwa na wakala wake.
Muktasari:
- Hata hivyo, mshambuliaji huyo aliweka wazi kuwa yuko tayari kuheshimu maamuzi ya kocha wake, akisisitiza kwamba kwake muhimu ni kuitumikia timu wakati wowote atakapopata nafasi, hata kama ni dakika chache tu.
Wakala wa mshambuliaji wa Manchester United, Benjamin Sesko, ameibua mjadala baada ya kupinga vikali jina la utani la ‘super sub’ linalotumiwa kumtaja mchezaji huyo, akisisitiza kuwa hafurahishwi na nafasi anayopata chini ya meneja Michael Carrick.
Sesko, aliyesajiliwa kwa dau linalokadiriwa kufikia Pauni 74 milioni akitokea RB Leipzig, ameanza kuonyesha makali yake katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu England (EPL), akifunga mabao tisa hadi sasa.
Kati ya mabao hayo, saba amefunga mwanzoni mwa mwaka huu, akionekana kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoimarika kwa kasi.
Licha ya kiwango hicho, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amekuwa akitumiwa zaidi kama mchezaji wa akiba, hali iliyomfanya kupewa jina la “super sub” kutokana na uwezo wake wa kubadilisha matokeo anapoingia kutokea benchi.
Katika mechi kadhaa, Sesko amekuwa na mchango mkubwa, akifunga mabao muhimu likiwemo la ushindi dhidi ya Fulham na Everton, sare ya dakika za mwisho dhidi ya West Ham, pamoja na bao la kufunga la ushindi dhidi ya Aston Villa yote akitokea benchi.
Hata hivyo, wakala wake Elvis Basanovic amesema wazi kuwa hapendezwi na jina hilo, akisisitiza kuwa mteja wake anastahili kuitwa “super striker” badala ya “Super sub”.
“Siipendi kabisa hiyo ‘super sub’. Naona ni bora aitwe ‘super striker’ kwa sababu ana uwezo kamili wa mshambuliaji,” amesema Basanovic.
Ameongeza kuwa Sesko ameanza mechi 13 na pia kuingia akitokea benchi mara 13, huku akifunga mabao kwa uwiano unaofanana katika nafasi zote mbili, jambo linaloonyesha ubora wake bila kujali anaanza au la.
Kwa sasa, kumekuwa na shinikizo kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wakimtaka Carrick kumpa nafasi zaidi ya kuanza kikosi cha kwanza, hasa kutokana na kiwango chake cha hivi karibuni.
Hata hivyo, chini ya Carrick, Sesko ameanza mechi chache tu licha ya mchango wake mkubwa.
Awali, mshambuliaji huyo aliweka wazi kuwa yuko tayari kuheshimu maamuzi ya kocha wake, akisisitiza kwamba kwake muhimu ni kuitumikia timu wakati wowote atakapopata nafasi, hata kama ni dakika chache tu.
Wakati huo huo, Manchester United imethibitisha kuwa mchezaji huyo amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika wiki za hivi karibuni, hali iliyomfanya ajitoe katika kikosi cha timu ya taifa ya Slovenia ili kupata muda wa kupona kikamilifu.
Licha ya changamoto hizo, Man United inaendelea kufanya vizuri katika msimamo wa ligi, ikishika nafasi ya tatu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Suala la nafasi ya Sesko linaendelea kuwa gumzo, huku wengi wakiamini kuwa ana uwezo wa kuwa mshambuliaji tegemeo ikiwa atapewa nafasi zaidi ya kuanza kikosi cha kwanza.