Mastaa Yanga wachimba mkwara!

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga usiku wa jana ililazimishwa sare ya 1-1 na KMC, lakini mapema mastaa wake wakiwasha moto kwa kuwachimba mkwara watetezi, Simba wasijidanganye, kwani watatulia tu mbele yao kwa madai hawana chao katika ligi ya msimu huu.

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga usiku wa jana ililazimishwa sare ya 1-1 na KMC, lakini mapema mastaa wake wakiwasha moto kwa kuwachimba mkwara watetezi, Simba wasijidanganye, kwani watatulia tu mbele yao kwa madai hawana chao katika ligi ya msimu huu.

Simba ipo nafasi ya tatu kwa kukusanya alama 46 ikiwa na mechi nyingi za viporo ambavyo zimekuwa zikiwapa kiburi mashabiki wao wakiamini wakivila vyote freshi wanaishusha Yanga kileleni na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.

Hata hivyo, kumbe nyota wa Jangwani wamekuwa wakisikia tambo hizo na juzi kati wamefunguka na kusema; “waacheni wachonge tu, lakini watatulia tu baadaye kwetu.”

Nahodha wa Yanga, Lamine Moro kwa niaba ya wachezaji wenzake aliliambia Mwanaspoti, wale wote wanaochonga dhidi ya timu yao wajiandae kuumbuka kwani, wanarejea kwenye Ligi Kuu Bara wakiwa moto ili kurejesha heshima yao.

Beki huyo wa kati alisema licha ya kutetereka kwenye mechi zao mbili za mwisho za ligi Kanda ya Kaskazini dhidi ya Coastal Union na Polisi, bado haiwafanyi iwatoe kwenye mbio zao za kuwania ubingwa msimu huu na kusisitiza, wanajua wapi pa kuwakamatia wapinzani wao katika mbio hizo.

Yanga ilinyooshwa na Coastal na kutibuliwa rekodi yao ya kucheza mechi 33 bila kupoteza kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Polisi na kumponza aliyekuwa kocha wao, Cedric Kaze, lakini Lamine alisema bado anaamini wana nafasi kubwa ya kubeba ubingwa hata kama kuna timu zina viporo.

Simba iliyotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ina mechi tano za viporo ambazo kama zote itashinda itawapa jumla ya pointi 15 zitakazowafanya wafikishe alama 61, huku Lamine anaamini wapinzani wao hao wana nafasi ya kuzitema baadhi ya pointi kwenye mech hizo za viporo.

“Tunasikia maneno mengi nje ya uwanja, lakini tuwaambie Yanga hatujalala licha ya mechi mbili zetu za mwisho kufanya vibaya na kuwatibua mashabiki wetu, tumejopanga na kumepania kurejea kwa nguvu bila kukata tamaa kwani tunaamini tuna nafsi ya kubeba ubingwa,” alisema Lamine.

“Tuna morali kubwa kwa sasa kuhakikisha tunashinda mechi zote ziliobaki. Hatujali kuangalia wapinzani wetu wanafanya nini bali kuhakikisha kila mechi tunavuna pointi tatu zitakazotupa majibu mwisho wa msimu.”

Beki mwingine wa kati, Bakar Mwamnyeto alisema, wao kama wachezaji wana mipango mikubwa ya msimu huu na moja ni kuhakikisha wanawalinda makipa wao ili kuhakikisha ndoto zao za ubingwa zinatimia.

“Ligi ni ngumu, lakini kama wachezaji wa Yanga tunayajua na kutambua majukumu yetu. Kama mabeki tukiwa imara hakuna mshambuliaji atakayemsumbua kipa weu, huku wenzetu kikosini wakikomaa mbele, tuna hakika ya kumaliza vyema mechi zilizosalia,” alisema Mwamnyeto.

“Tukipambana tushinda michezo yote ni nafasi kwetu kwa kuwa ubingwa, kwani kwa sasa hakuna mwenye uhakika nao, nafasi ipo kwa wote cha muhimu kwetu ni kupambana na kujituma na ndio lengo letu wachezaji.”

Ukiondoa mchezo wa jana dhidi ya KMC, Yanga imesaliwa michezo 10 kabla ya kumaliza msimu, huku pia ikiwa na kazi kwenye michezo minne ya Kombe la Shirikisho (ASFC) hadi kufika fainali ikiwamo mechi yao ya raundi ya 16 Bora dhidi ya Tanzania Prisons itakayopigwa Aprili 30.

Imeandikwa na Khatimu Naheka, Clezencia Tryphone, Olipa Assa na Oliver Albert