Matola, Mgunda kuonyeshana ubabe Simba ikiivaa Namungo FC Ligi Kuu
Muktasari:
- Simba inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi tatu wakati huo namungo FC ikishika nafasi ya tano ikiwa na pointi nne.
Makocha wawili ambao wamewahi kufanya kazi pamoja katika klabu na timu ya taifa 'Taifa Stars', Selemani Matola na Juma Mgunda leo watakuwa na kibarua cha kuonyesha nani zaidi baina yao wakati Simba itakapoikaribisha Namungo FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:15 usiku.
Matola atakuwa anakiongoza kikosi cha Simba wakati huo Mgunda akiwa Kocha Mkuu wa Namungo FC.
Simba baada ya kufuzu hatua ya pili ya mtaono wa Ligi ya Mabingwa, inarudi kwenye ligi ukiwa ni mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki, huku Simba ikiwa imecheza mchezo mmoja na kupata ushindi Namungo imeshinda mmoja na kutoka sare mmoja.
Rekodi zinaonyesha kuwa ni mchezo mgumu kwa kuwa wanakutana makocha wawili wanaojuana Juma Mgunda aliwahi kuwa kocha mkuu wa muda wa Simba huku msaidizi wake akiwa Matola ambapo leo wote wawili watakuwa kwenye mabenchi wakizisimamia timu zao.
Msimu uliopita Simba ilifanikiwa kuchukua pointi sita na mabao sita kwenye michezo miwili dhidi ya Namungo baada ya kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex na kupata idadi hiyo kwenye mchezo wa pili Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Mkoani Lindi.
Katika mchezo uliopita Namungo ilitoka sare dhidi ya Pamba na mchezo wa pili ikaichapa Prisons bao 1-0, huku Simba ikishinda 3-0 dhidi ya Fountain.
Akizungumzia mchezo huo Matola amesema mechi hiyo haitakuwa rahisi kwani Namungo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kwenye mechi za hivi karibuni.
"Tunarajia kuwa na mechi ngumu kama mkiangalia rekodi, Namungo wamekuwa wakitusumbua licha ya kuwafunga mechi mbili za mwisho, wana kocha mzuri anayeijua Simba, tutaingia na tahadhari kubwa," amesema Matola.
Mgunda akizungumzia mchezo huo alisema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kushindana na Simba huku wakitarajia mchezo mgumu wakitambua wanakwenda kukutana na timu ngumu.
"Tuna siku tatu hapa mjini, tumejiandaa vizuri kuja kukutana na timu nzuri, yenye wachezaji wazuri, maandalizi yote tumeyafanya ili tufanye vizuri, tuhaiheshimu Simba tumekuja kushindana nao,"amesema Mgunda.
Mechi 12 zilizopita Simba na Namungo
19.02.2025 Namungo 0-3 Simba
25.10.2024 Simba 3-0 Namungo
30.04.2024 Namungo 2-2 Simba
09.11.2023 Simba 1-1 Namungo
03.05.2023 Namungo 1-1 Simba
16.11.2022 Simba 1-0 Namungo
03.05.2022 Namungo 2-2 Simba
03.11.2021 Simba 1-0 Namungo
18.07.2021 Simba 4-0 Namungo
29.05.2021 Namungo 1-3 Simba
08.07.2020 Namungo 0-0 Simba
29.01.2020 Simba 3-2 Namungo