Mayele awatumia meseji mabeki Ligi Kuu

MZEE wa kutetema, Fiston Mayele ndo ameshasema hivyo na sasa wapinzani wajipange. Straika huyo wa mabao amepiga stori na Mwanaspoti na kueleza namna Yanga wanavyolitaka kombe la Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akiahidi mabao makali zaidi ya lile la kuombea mkopo benki alilofunga juzi kwa tik-taka dhidi ya Biashara United.

Mayele amesema malengo yake makubwa ni kuhakikisha Yanga inafanya vizuri na kuchukua makombe yote yaliyo mbele yao na anashukuru walianza vyema kampeni hiyo baada ya kubeba Ngao ya Jamii wakiwabwaga mahasimu wao Simba kwa 1-0, bao alilotupia kambani yeye mwenyewe aliposimamia shoo ya mauaji.

Straika huyo ameongeza kwamba lengo lake la kwanza ni kuona Yanga inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambao wameukosa kwa kwa misimu minne mfululizo na pia kubeba ndoo ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na baada ya hapo ndio mengine yatafuata ikiwamo kusaka tuzo binafsi.

“Kati ya mambo ambayo yatafuata baada ya hapo nitaangalia mafanikio yangu binafsi kama kutwaa tuzo ya mfungaji bora na tuzo nyingine za hapa ndani,” alisema Mayele na kuongeza;

“Wakati natoka DR Congo nilikuwa miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri kule na nilitegemewa kulifanya hilo hapa Yanga, nashukuru mwanzo wangu si mbaya mpaka sasa nimefunga mabao manne ila mwisho wa msimu nina imani nitaibuka kinara wa mabao.

“Kama nikiweza kufunga katika kila mechi iliyo mbele yetu maana yake nitaisaidia timu kufanya vizuri na kufikia yale malengo yake tuliyopanga kabla ya msimu kuanza.”

Mayele alifunga bao kali la kusawazisha wakati Yanga ikiwa imetanguliwa 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa juzi, akitumia vyema krosi ya mguu wa kushoto kutoka kwa beki wa kulia anayepanda mbele kusaidia mashambulizi, Djuma Shabani.

Straika huyo Mkongomani alibinuka tik-taka mbele ya Feisal Salum ambaye pia alijaribu kufunga kwa staili hiyo hiyo, lakini aliukosa mpira ambao ulitua mguuni mwa mdunguaji huyo aliyeuweka wavuni mpira.

Bao hilo lilikuwa ni kama marudio ya bao alilofunga kwa tik-taka katika mechi ya kirafiki ambayo Yanga walishinda 2-1 dhidi ya KMKM kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar Novemba 21, 2021.

Kwenye mchezo huo wa kirafiki, bao la Mayele lilitokana na kona iliyopigwa na Jesus Moloko iliyokwenda kwenye kichwa cha Yanick Bangala aliyetoa pasi kwa straika huyo wa mabao ambaye alikuwa amelipa goli mgongo lakini haraka alibinuka tik-taka na kuweka bao tamu la kideoni kambani.

Mayele ameshathibitisha ni mkali wa kufunga mabao matamu ya kideoni kwani alianza makali hayo tangu alipokuja nchini kwa mara ya kwanza akiwa na timu ya taifa ya DR Congo kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Januari 12, 2021, mechi iliyotumika kumuaga nahodha, Aggrey Morris.

Kwenye mchezo huo Mayele alijitambulisha kwa mara ya kwanza nchini baada ya kufunga bao katika dakika 18, akipokea pasi kutoka kwa Luzolo huku akiwa amelipa goli mgongo, aligeuka na kupiga shuti kimo cha mbuzi lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Baada ya Yanga kumsajili, mechi yake ya kwanza ya kimashindano nchini ilikuwa ni ile dhidi ya Simba ambayo alifunga bao tamu lililofanana kiasi na lile aliloifungia timu yake ya taifa dhidi ya Stars.

Bao lililoizamisha Simba lilitokana na mpira mrefu kutoka kwa kipa Djugui Diarra kwenda kwa Farid Mussa aliyepiga pasi ya mwisho kwa Mayele akiwa analiangalia goli kwa pembeni, akapiga shuti bila kuutuliza mpira uliokwenda kumshinda Aishi Manula na kuingia kimiani.

Mkali huyo wa kutupia mabao alifunga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, bao lilitokana na mpira wa krosi kutoka kwa Kibwana Shomary, kisha Mayele kupita nyuma ya Daniel Amoah mbele ya Yvan Mballa na kuunganisha mpira huo.

Katika mechi ya KMC, alifunga bao jingine kwenye ligi baada ya Feisal Salum kupiga shuti kali, huku mabeki wa wakidhani Mayele ameotea alikwenda kuugusa mpira huo na kumshinda Farouk Shikhalo kuzama moja kwa moja nyavuni.

Bao lake la tatu lilikuwa mechi ya ugenini dhidi ya Mbeya Kwanza alipokea mpira mrefu kutoka kwa Bakari Mwamnyeto, alituliza mpira na kumpa Saido Ntibazonkiza, aliyepenyeza pasi kwa Feisal Salum, aliyepiga pasi ya chichini ndani ya boksi na kumkuta Mayele.