Mbappe akabidhiwa chumba maalumu Madrid

Muktasari:
- Mbappe alijiunga na Real Madrid kama mchezaji huru huru baada ya mkataba wake PSG kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita, lakini ada yake ya usajili ikivunja rekodi.
Madrid. Mshambuliaji mpya wa Real Madrid, Kylian Mbappe ameduwazwa baada ya kukabidhiwa chumba maalumu chenye hadhi ya nyota tano huko kwenye uwanja wa mazoezi wa Madrid, ambacho atakitumia kwa ajili ya kupumzika na shughuli nyingine.
Winga huyo wa zamani wa Paris-Saint Germain amepewa chumba hicho chenye kibaraza kinachoangalia eneo la viwanja vya mazoezi vya Real Madrid, ambapo eneo hilo lilijengwa kwa zaidi ya Pauni 100 milioni.
Mbappe, 25, alijiunga na miamba hiyo ya Ulaya kama mchezaji huru baada ya mkataba wake PSG kumalizika, lakini pesa aliyolipwa kwa ajili ya usajili kama mchezaji huru, imeweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyelipwa ada kubwa zaidi ya usajili kwenye historia ya mchezo wa soka.
Real Madrid imekuwa na kawaida ya kugawa vyumba vyenye hadhi ya juu kwa mastaa wake katika eneo hilo la mazoezi, ambapo kila mchezaji anakuwa kwenye chumba chake binafsi, ambapo hata milango inafunguka kwa alama za vidole za mchezaji husika.
Ndani ya jumba hilo linalofanana na hoteli ya nyota tano kuna mabwawa ya kuogelea, vyumba vya michezo ya kompyuta, sinema na vyumba vingine 57 huku jengo hilo likijengwa kwenye eneo linalozidi mita za mraba 7,800. Mbappe anakaa chumba namba 103.
Eneo hilo la mazoezi la Valdebebas Park lilifunguliwa mwaka 2005 na linaripotiwa kugharimu Pauni 100 milioni.
Mbappe aliripotiwa kuchukua chumba ambacho awali alikuwa akikaa kiungo Toni Kroos ambaye ametangaza kutundika daluga baada ya Euro 2024 kumalizika.